Na Albert Kawogo
MGOMBEA Mwenza, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amepokewa kwa shangwe na wakazi wa Kata ya Langabilili, wilaya ya Itilima mkoani Simiyu jana Jumanne Septemba 2, 2025 alipowasili mkoani humo.
Akiwa ametokea mkoa wa Mara, Dkt. Nchimbi ameingia Simiyu kuendelea na mikutano ya kampeni na tayari ameendesha mikutano majimbo ya Busega, Bariadi Vijijini na sasa ameingia jimbo la Itilima.

Akiwahutubia wananchi katika stendi ya Mabasi ya Langabilili, Balozi Dkt.Nchimbi alitumia nafasi hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Itilima, Njalu Daudi Silanga sanjari na Wagombea Ubunge wengine pamoja na Madiwani wa Mkoa huo.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Nchimbi ameinadi Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 ambayo kimsingi imelenga kwenda kuboresha maisha ya wananchi na ustawi wa Maendeleo katika miaka mitano ijayo, huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumchagua mgombea Urais wa CCM Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa chama hicho.
Dkt. Nchimbi anaendelea na kampeni zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huku akinadi Sera na Ilani ya chama hicho 2025-2030 kwa Wananchi, ikiwa ni katika harakati za kuomba ridhaa ya Watanzania kuwaongoza katika awamu nyingine ya miaka mitano, katika Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
