Airtel Tanzania kuongeza uwekezaji

0

Na Mwandishi wa OMH

SERIKALI ya Tanzania na uongozi wa kampuni ya simu ya Airtel duniani wameafikiana kuongeza kiwango cha uwekezaji katika kampuni ya Airtel Tanzania, kwa lengo la kuimarisha ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

Ikumbukwe kuwa Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inamiliki asilimia 49 ya hisa katika kampuni ya Airtel Tanzania, ambapo umiliki huu mkubwa unaiwezesha Serikali kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kimkakati.

Akizungumza na waandishi wahabari Jumatano, Agosti 13 ,2025, jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema wamekubaliana kuwekeza kwenye mkongo wa Taifa na kuongeza bidha mpya ‘new products’.

“Ni dhamira yetu kuona sambamba na kuwa na mtandao imara nchi nzima, Airtel Tanzania inakuwa na bidhaa ambazo zitawawezesha watanzania kutumia zaidi mifumo ya teknolojia, mbali na malipo ya pesa,” alisema Mchechu.

Mchechu alizungumza hayo muda mfupi baada ya kufanya mkutano wa ndani na timu ya viongozi wa Airtel ikiongozwa na mwanzilishi na Mwenyekiti wa kampuni hiyo ulimwenguni, Sunil Bharti Mittal.

Alisema, menejimenti ya Airtel imeelekezwa kupitia mpango mkakati wake ili uendane na ndoto pana ya nchi ya kuleta mageuzi katika sekta ya mawasiliano na kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inachangia ipasavyo kwenye pato la taifa kupitia gawio, ajira, na ulipaji wa kodi.

“Kile ambacho menejimenti ya kampuni ya Airtel itachakata na kukileta kwetu kama wanahisa, tutaunga mkono— iwe ni kupitia faida tunayopata ndani ya Airtel, mikopo au kwa kuweka mtaji ‘hela zetu wenyewe,” alisema Mchechu.

Kwa upande wake Mitta, alisema kupitia uwekezaji katika eneo la kidigitali, kampuni ya Airtel duniani itahakikisha inaisaidia serikali kutekeleza Dira 2050.

Kwa mujibu wa Dira 2050, Serikali imedhamiria kuwa na uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050, huku pato la Taifa likifikia $1 trilioni na pato la mtu mmoja mmoja $7000 kwa mwaka.

“Tanzania imedhamiria kutekeleza Dira 2050 na ili kufanikiwa lazima kufanya mageuzi ya kidijitali. Tuko tayari kuisaidia Tanzania kwani tunajivunia kuwekeza katika nchi hii,” alisema Mitta.

Katika mkutano na Msajili wa Hazina Bw. Mitta aliambatana na Sunil Kumar Taldar, Afisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Afrika, Apoorva Mehrotra, Mkurugenzi wa Airtel Afrika Mashariki, Eliudi Betri Sanga, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania.

Wengine ni Adolph Timoth Kasegenya, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Money, Charles Mustafa Kamoto –Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania na Beatrice Singano –Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here