Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema viongozi wa ACT Wazalendo wanadanganya wananchi kuhusiana na takwimu za ukuaji uchumi katika mikutano yao na kimebainisha kuwa hata kwa macho maendeleo yanaonekana.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Zanzibar Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, ni aibu kiongozi kudanganya.
Mbeto alibainisha kuwa, hakuna wakati uchumi wa Zanzibar umekuwa vizuri kama wakati huu wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Alisema, jambo la kushangaza Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman ‘OMO’, hivi karibuni akiwa Uzi alidai, uchumi wa Zanzibar haupo vizuri kutokana na kutokuwepo kwa biashara.
“Mtu huyo anasema hakuna biashara kisha anadai nje ya bandari kuna meli zimesongamana zinasubiri kuingia,” alisema Mbeto na kuhoji, “iwapo Zanzibar hakuna biashara, hizo meli zitakuwa zimebeba nini?”
Alisema, kwa mwaka Zanzibar inapata gawio la Shilingi Bilioni 21 kutoka makampuni ya simu na sio kweli kuwa kampuni hizo hazilipi chochote Hazina ya SMZ, kama wanavyodai.
Alibainisha kuwa, kitu ambacho Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu na Mwenyekiti wake OMO hawazungumzii, ukuaji wa sekta ya utalii nchini ambayo inafanya ndege za Kimataifa zaidi ya 50 kutua kila siku Zanzibar na kufanya ndio kiwanja cha ndege bora kuliko vingine vyote nchini,” alisema.
Mbeto anadai, OMO anatoa kauli za uongo kwa wananchi wa Uzi ambao maendeleo wanayaona kwa macho yao, kwani toka kuumbwa ulimwengu kwa mara ya kwanza wanapata daraja na barabara ya lami yenye urefu wa Kilometa 3.5.
“Zingine chuki binafsi, viashiria vya ukuaji uchumi vipo wazi, leo wafanyakazi serikalini kuanzia tarehe 18 wanaanza kupata mshahara na haizidi tarehe 23 na hakuna mradi ambao umesimama kutokana na ukosefu wa fedha,” alibainisha Mbeto.
Alisema, Zanzibar ni kisiwa na njia zake kuu ni bandari na viwanja vya ndege na ili kuvutia uwekezaji na utalii, Rais Mwinyi aliamua kuboresha na kujenga bandari za boti za abiria na mizigo sanjari na ujenzi wa barabara za lami kwenda maeneo ya uwekezaji.
“Hadi 2030 nakuhakikishia hakutakuwa na barabara ya vumbi Zanzibar,” alisema, mwenezi Mbeto.
Mbeto alisema, ada, tozo, fedha zinazolipiwa viza zote zinaingia hazina ya Zanzibar achilia mbali fedha zingine wanazotumia wanapopata huduma mbalimbali wawapo nchini.
“Mwekezaji anapokuja anaangalia, sera ni rafiki? Miundombinu ya barabara ikoje? Bandari, viwanja vya ndege ambako Terminal II imejengwa, miji ya kisasa na huduma zingine vimevutia zaidi ya makampuni 451 kuja kuwekeza Zanzibar,” alisema Mwenezi Mbeto.