Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI
WANANCHI zaidi ya 9000 waliotembelea banda la Ofisi ya Rais -TAMISEMI wakati wa Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea jijini Dodoma, wamehudumiwa moja kwa moja kwa kupewa elimu, huduma na ufafanuzi wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya serikali kupitia Ofisi ya Rais -TAMISEMI.
Ofisi ya Rais – TAMISEMI inayowahudumia wananchi kupitia mikoa na halmashauri imetumia jukwaa hilo muhimu kuwasogezea wananchi huduma ya elimu kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Sanjari na hilo, imetoa elimu ya matumizi ya Mfumo wa TAUSI, mwongozo wa ununuzi wa viwanja ikiwa ni pamoja na masuala mengine yanayosimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Akizungumza katika maonesho hayo, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia TAMISEMI, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Sospeter Mtwale, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma, akibainisha kwamba ofisi hiyo itaendelea kuwa kiunganishi muhimu kati ya serikali kuu na wizara mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati.