Wananchi wafurahishwa na uwazi wa huduma kupitia mfumo wa Tausi

0

Na Angela Msimbira, OR-TAMISEMI

WANANCHI wa Mkoa wa Dodoma wameipongeza Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuanzisha matumizi ya Mfumo wa Tausi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, wakisema umeleta mapinduzi katika utoaji wa huduma bora kwa jamii, hususani upatikanaji wa viwanja.

Wakizungumza walipotembelea banda la TAMISEMI katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika Nzuguni, Jijini Dodoma, wananchi hao walisema mfumo huo umeongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi mkubwa katika huduma zinazogusa maisha yao moja kwa moja.

Subira Mwasiti, mkazi wa Iyumbu, alisema kuwa awali kulikuwa na changamoto nyingi katika kupata viwanja, lakini sasa hali imebadilika.

“Kupitia mfumo wa Tausi, kila kitu kiko wazi – kuanzia eneo lilipo, gharama, hadi taratibu za ununuzi. Hakuna tena upendeleo wala ucheleweshaji wa makusudi,” alisema.

Naye Mwita Damiani kutoka TAMISEMI alisema mfumo huo umeongeza imani ya wananchi kwa Serikali kwa kuwa taarifa zote muhimu sasa zinapatikana kwa uwazi na kwa wakati.

“Awali kulikuwa na hofu juu ya upotevu au ugawaji wa viwanja kwa upendeleo, lakini sasa kila kitu kinapatikana kwa uwazi. Halmashauri zinakuwa na rekodi sahihi za waliopata viwanja, mapato na taratibu zote za manunuzi,” alisema.

Mfumo wa Tausi hutumika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na umeunganishwa na mifumo mingine ya Serikali katika sekta za afya, elimu, mipango miji na ardhi.

Kwa mujibu wa wananchi, mafanikio haya yanapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha huduma za serikali zinapatikana kwa uwazi, ufanisi na bila urasimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here