Prof. Kabudi awapongeza watendaji wa WMA

0

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi ametembelea Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya NaneNane Dodoma na kuwapongeza watendaji wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Kabudi amesema, WMA ni miongoni mwa Taasisi muhimu za Serikali zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Ametoa rai kwa watendaji wa WMA kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuwalinda walaji katika sekta zote nchini wakiwemo wakulima kupitia jukumu lao kuu la uhakiki wa vipimo.

Mbali na Prof. Kabudi, wananchi mbalimbali wameendelea kutembelea Banda la WMA na kupatiwa elimu ya vipimo.

Pamoja na kupatiwa elimu ya vipimo, wananchi hao wanapata fursa ya kuuliza maswali ana kwa ana na kujibiwa na wataalamu pamoja na kuelekezwa kwa vitendo namna WMA inavyohakiki vipimo mbalimbali ili kumlinda mlaji.

Miongoni mwa waliofika leo, Agosti 8, 2025 na kupatiwa elimu hiyo ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Brother Martin ya mkoani Dodoma, ambapo walipokewa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Wakala wa Vipimo (WMA) Veronica Simba.

Veronica alisema, moja ya mikakati ya wakala huo katika kupanua wigo wa utoaji elimu ya vipimo, ni kuanzisha vilabu (clubs) za vipimo katika shule mbalimbali nchini ili kuwajengea uelewa wanafunzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here