Na Mwandishi Wetu, Same
MAAFISA 35 na Askari 144 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini wamepandishwa vyeo katika hafla ya heshima iliyofanyika jana katika viwanja vya ofisi za TFS mjini Same, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mathew Kiondo ambaye ni Kamanda wa TFS Kanda ya Kati aliwapongeza watumishi hao kwa utendaji bora, uadilifu na kujituma katika kulinda rasilimali za misitu na nyuki.
Alisisitiza kuwa kupandishwa vyeo ni heshima inayokuja na wajibu mkubwa.
βPandisho la cheo si tu zawadi, bali ni dhamana. Tuwe waadilifu, tushirikiane na wananchi, na tuendelee kusimamia misingi ya Jeshi la Uhifadhi,β alisema Kamishna Kiondo.
Alisisitiza umuhimu wa askari na maafisa hao kusoma na kuelewa Kanuni za Jumla za Jeshi la Uhifadhi (GOs) ili kutambua vyema majukumu na mipaka ya madaraka yao.
Katika hotuba yake, Kiondo alikumbusha kuwa TFS inazidi kujipambanua kitaifa kama taasisi ya mfano katika usimamizi endelevu wa misitu, ikiwa na malengo ya kukuza uchumi wa kijani na kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni Kamanda wa TFS Kanda ya Kaskazini, James Nshare, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Jimson Mhagama, Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), pamoja na wawakilishi kutoka TANAPA, TAWA na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Katika salamu zake, Mkurugenzi wa Halmashauri aliishukuru TFS kwa ushirikiano thabiti na kueleza kuwa mafanikio ya usimamizi wa misitu yanategemea ushirikiano baina ya taasisi na mamlaka za halmashauri, kwa kuwa misitu mingi ipo katika maeneo yao ya kiutendaji.
Hafla hiyo ilipambwa na burudani fupi, pongezi kwa waliopandishwa vyeo, na hotuba za hamasa kutoka kwa viongozi mbalimbali waliotoa wito wa kuendeleza mshikamano katika utunzaji wa rasilimali za taifa.