Mbeto awajibu ACT kuhusu marufuku ya matangazo ya karatasi ya wagombea

0

AGIZO la kupiga marufuku matangazo ya wagombea ya karatasi katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja ni la kwake aliyelitoa kwa mamlaka aliyopewa na Sheria namba 7 ya Serikali za mitaa na Manispaa.

Akizungumza kufuatia malalamiko ya ACT Wazalendo kuwa marufuku ya matangazo ya wagombea ya karatasi ni agizo la CCM, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Mbeto Khamis Mbeto alisema si kweli.

“Mkuu wa Mkoa ni mteule wa Rais na sio chama hivyo hatuna mamlaka nae kwani pia anaongozwa na sheria za mamlaka ya halmashauri za miji na manispaa,” alisema Mbeto.

Alibainisha, Manispaa na halmashauri zimepewa mamlaka ya kupanga miji kulingana na sheria hiyo na mkuu wa mkoa ni sehemu ya mamlaka hiyo.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja Idrisa Kitwana Mustafa alipiga marufuku maeneo yote mkoani humo matangazo ya wagombea ya karatasi ili kulinda haiba ya mji huo.

Mkuu wa Mkoa huyo alitaka kutumika kwa matangazo ya kidigitali ili kuondokana na uchafuzi wa mazingira na kuwataka wagombea kujiandaa kidigitali.

Mwanasheria wa ACT Wazalendo, Omary Said Shaaban katika mkutano na wanahabari hivi karibuni, alilalamikia hatua hiyo ya mkuu wa mkoa na kushangaa CCM kukaa kimya.

Mwanasheria huyo alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa mkuu huyo wa mkoa anatekeleza agizo la CCM jambo ambalo Mbeto alisema halina mantiki.

Mbeto alisema, CCM ni chama kikubwa kina wagombea wengi hivyo agizo hilo la RC linawagusa hata wao kwani wana wawakilishi wao wenye uwezo mdogo kifedha kumudu matangazo ya namna hiyo.

“Sisi ni wadau tu wa uchaguzi mkuu tunasubiri tamko kutoka kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwani wao pia wana sheria zinazo viongoza vyama kuhusiana na matangazo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here