Rais Mwinyi: Zanzibar itaendelea kuwa daraja katika kuimarisha elimu ya juu

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Zanzibar itaendelea kuwa daraja muhimu la kuiunganisha Afrika na ulimwengu katika masuala ya ubunifu, tafiti na uimarishaji endelevu wa elimu ya juu kwa ajili ya maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Mkutano wa Elimu ya Juu na Teknolojia Afrika (QS AFRICA FORUM 2025) uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege tarehe 3 Julai 2025.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa jambo muhimu ni kuwa na ushirikiano na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu barani Afrika na duniani, ili kutoa fursa ya kuunganishwa kwa vyuo kwa ajili ya kufanya tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuimarisha elimu ya juu.

Akizungumzia suala la teknolojia ya akili mnemba (AI), Rais Dkt. Mwinyi alisema, Zanzibar haipaswi kubaki nyuma katika matumizi ya teknolojia hiyo, lakini ni lazima ihakikishe kuwa inapata manufaa na faida zake, sambamba na kuhakikisha udhibiti wa athari zake kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa za kielimu.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali ya Zanzibar imeipa sekta ya elimu, hususan elimu ya juu, kipaumbele katika kuleta maendeleo, kukuza fursa za kiuchumi na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi.

Amehitimisha kwa kueleza kuwa kufanyika kwa mkutano huo hapa nchini ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika, na kuwa ni jukwaa la kutoa sauti ya pamoja kuelekea maendeleo endelevu ya elimu ya juu, ubunifu na teknolojia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here