Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuichangamkia siku ya leo ambayo ni ya mwisho kwa wenye nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu ujao hapo Oktoba mwaka 2025.
Akizungumza na wanahabari mjini Zanzibar jana, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis kitendo tu cha kuchukua fomu ya kuwania Ubunge, Uwakilishi au Udiwani CCM ni ujasiri kwa mwanachama.
Alisema, wenye nia watumie saa chache zilizobaki kuchukua na kurudisha fomu kwani hata kama hawatapendekezwa watakuwa wamekichangia chama.
“Hivi sasa chama kinaenda kwenye uchaguzi mkuu, kuna mambo mengi ikiwa ni pamoja na vikao, mikutano ya kampeni vyote hivyo vinahitaji pesa” alisema Mbeto.
Pesa hizo wanazotoa kuchukua fomu ni kukichangia chama chao hata kama hawapita kwenye uteuzi, hivyo wasiogope waendelee kujitokeza na kuchukua fomu.
Mbeto amewataka watia nia watumie haki yao ya kikatiba kwani chama hakina mwenyewe ili mradi ni MwanaCCM, mwenye akili timamu anayejua kusoma na kuandika Kiswahili kwa ufasaha.
“Katika uteuzi sisi tutaangalia sifa za wanachama ikiwa ni pamoja na uadilifu na uaminifu wake” alisema.
Alibainisha kuwa, wingi wa watu kuchukua fomu inaonyesha jinsi chama kinavyokubalika na ndio maana wao waenezi wanasema ‘Ushindi Lazima’.
Mbeto aliwatahadharisha WanaCCM kuwa hakuna ambaye ametumwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi au Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika mkutano maalum Dodoma, Mama Samia na Dkt. Mwinyi walisema hawajamtuma mtu na kama kuna wanayemtaka wana nafasi zao 10 za uteuzi” alisema Mbeto.
Mwenezi huyo alisema, mtu ambaye anajinasibu kuwa katumwa na kiongozi wa juu huyo hafai, hajiamini na hajielewi, hivyo hafai kupewa dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Mbeto alisema, hata wanaofikiri kuwa wanawania nafasi hizo kwa ajili ya maslahi ya kifedha nao wanapotea, hawawezi kufikia malengo wanayotarajia, kwani kiasi wanacholipwa ni kidogo sana.
“Kama ni kuwatumkia wananchi fedha wanazopata madiwani, wabunge na wawakilishi ni kidogo sana ila kama mtu yupo kwa ajili ya familia yake, sawa ni pesa nyingi” alisema.
Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu ndani ya CCM linatarajiwa kuhitimishwa leo Julai 2, saa 10 alasiri.