Na Jumbe Abdallah
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeonyesha wazi kuumizwa na kitendo cha wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini vikiwemo vya upinzani kujitokeza kuwania nafasi za ubunge na udiwani kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Hivi sasa, kwenye mitandao ya kijamii na hata mitaani, gumzo ni idadi kubwa ya wanachama wa vyama vya siasa waliojitokeza kuchukua fomu, huku wengine wakitangaza nia ya kujitosa kugombea nafasi hizo kwa tiketi ya vyama mbalimbali vinavyoshiriki uchaguzi.
Jambo hilo, limeonekana kukivuruga Chadema ambacho kiliamini kwasababu ya kukosekana kwa ushiriki wao, uchaguzi wa mwaka huu utapoteza mvuto na utakosa idadi kubwa ya wataochukua fomu ya kugombea nafasi mbalimbali, lakini hali imekuwa tofauti.
Kupitia barua yake aliyoiandika na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii, jana Julai 1, 2025 mmoja wa viongozi wa chama hicho Godbless Lema, alielezea jinsi wanavyoumizwa na kitendo cha watu hususani vijana, kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi ujao.
“Kwa heshima na taadhima ninawaandikia barua hii nikiwa mwenye uchungu wa kweli juu ya hatma ya nchi yetu…” aliandika Lema, na kuelezea kuhusu madai yao ambayo waliyatoa kuhusu mwenendo wa uchaguzi nchini na maamuzi yao ya kuzuia uchaguzi kwa kutumia mkakati wao wa No reform, no Election.
Kupitia barua hiyo Lema alisema, wakati wao wakipambana kuhakikisha wanazuia uchaguzi, wanaibuka watu wanachukua fomu za kugombea nafasi za uongozi wakiwemo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wengine kutoka vyama vya upinzani ambao wanaonyesha nia ya kugombea.
“Kinachoumiza zaidi ni hiki; wakati Chadema wanasimama imara kwa jili ya Taifa, wimbi kubwa la watu, hasa vijana linakimbilia kuchukua fomu za kugombea. Wanaona kutokuwepo kwa Chadema kama fursa ya kupenya bila ushindani,” aliandika Lema.
Aliendelea “Sisi (akimaanisha wananchi, vijana) ndio tulipaswa kuwa mstari wa mbele kulinda msingi wa “No reform no election. Sisi ndio tungepaswa kulia na kudai tume huru. Tungepaswa kuandika, kuandamana, kuhamasisha na kushinikiza mageuzi ya kweli kisiasa.”
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na Afrika Leo, wamesema hatua hiyo ya idadi kubwa ya vijana kuingia kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu ujao, ni pigo kubwa kwa Chadema ambao wamekuwa wakilitegemea kundi hilo kufanikisha harakati zao za kisiasa.
“Ngome na tegemeo kubwa la Chadema kwa miaka mingi ni vijana; wao ndio wamekuwa wakikipambania chama chao mitandaoni na mitaani, kwa miaka ya nyuma kundi hilo ndilo lilikuwa linajitokeza kwa wingi kwenye maandamano yanayoitishwa na chama hicho, sasa vijana hao hao wameamua kujitokeza kuwania uongozi, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa Chadema,” alisema David Isaya.
Alisema, pigo la kwanza ambalo walilipata Chadema, ni kitendo cha vyama takribani 17 vya upinzani kukubali kushiriki uchaguzi, jambo ambalo halikutarajiwa, kwani chama hicho kikuu cha upinzani kiliamini msimamo wao wa kuzuia uchaguzi, ungeungwa mkono na vyama vingine.
“Mpango wa kuzuia uchaguzi, Chadema hawakuutafakari kwa kina na waliamini ungeungwa mkono, lakini kitendo cha vyama vingine vya upinzani kutangaza kushiriki uchaguzi, umepunguza nguvu ya agenda yao, lakini kubwa zaidi ni mwitikio huu wa watu kujitokeza kwa wingi kugombea, ni dalili za wazi za kukwama kwa mkakati wao,” alisema.
Aidha, uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, idadi kubwa ya wanachama wa Chadema ukiachilia mbali wale ambao tayari wameshajiunga na vyama vingine kikiwemo CCM, ACT Wazalendo, CUF, CHAUMMA na vinginevyo, wanajipanga kukihama chama hicho.
Mmoja wa vijana hao wa Chadema, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini alisema, yeye ni mmoja wa wanachama wa chama hicho ambaye amepanga kuhama ili apate fursa ya kugombea udiwani kwenye Kata anayoishi.
“Nimeishi hapa kwa miaka mingi sana, nimejijenga kisiasa vya kutosha, wananchi wa hapa kwa muda mrefu wameniomba nigombee ili niwasaidie kupigania changamoto zinazowakabili, mwaka huu nikaweka wazi mapema kwamba nitagombea, lakini ghafla chama changu kikaonyesha wazi hakipo tayari kuingia kwenye uchaguzi,”
“Nisisitize msimamo wangu, nipo tayari kugombea, wananchi ambao wengine nimeishi nao tangu nikiwa mdogo wapo tayari niwe kiongozi wao, chama hakiwezi kuwa kikwazo, wamekubali nihame na wakati wowote nitatangaza mwelekeo wangu mpya, nao wamesema wataniunga mkono huko nitakapokwenda,” alisema.
Mbali na kundi hilo, wapo madiwani wa Chadema ambao walishinda kwenye Kata mbalimbali na bado wana kiu ya kuwatumikia wananchi wao, nao wamepanga kukihama chama hicho na kwenda kwenye vyama vingine ili kutetea nafasi zao.
“Ndio maana umeona wale wabunge 19 wakiongozwa na Mdee nao wametimkia kwenye vyama vingine kikiwemo ACT Wazalendo, bado wanataka kuisaidia nchi, lakini wananyimwa nafasi hiyo na msimamo wa chama chetu, wapo wengi wenye misimamo hiyo na watahama, ni suala la muda,” alisema mwanachama mwingine wa Chadema.
Alisema, uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi haukuwa sahihi, kwani chama cha siasa kinapokosa uwakilishi kwenye ngazi kuanzia mtaa, udiwani na ubunge kwa miaka mitano, kinakuwa hatarini.
“Kwasasa chama kimezuiwa kufanya siasa, hapo hapo tumepoteza sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu, baada ya miaka mitano tutakuwa kwenye hali gani kisiasa na kiuchumi? Maana hatutakuwa na ruzuku, hatutakuwa na sauti bungeni wala kwenye maeneo ambako kuna wananchi,”
“Viongozi wetu hawakufikiria vizuri, walifanya maamuzi kwa mihemko wakiamini wataungwa mkono, matokeo yake wamekigharimu chama hiki ambacho tumekipigania kwa jasho na damu; kila kukicha badala ya kujenga chama tunaendelea kuongeza kesi za kufungua na kufunguliwa,” alisema kwa masikitiko mwanachama huyo.
Aidha, wanachama wa Chadema wameelezea masikitiko yao kwa kile kinachoendelea kwenye makundi ya mitandao ya kijamii ya chama hicho, ambapo tangu uchaguzi ulipokwisha, makundi yameendelea kusigana na mpasuko unaendelea kila kukicha.