Mauzo ya biashara ya mazao ya misitu na nyuki nje ya nchi yaongezeka

0

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imebainisha mafanikio makubwa katika biashara ya mazao ya misitu na nyuki nchini, ikiwemo ongezeko la uzalishaji, viwanda na mauzo nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati unaofanywa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Akizungumza leo Mei 19, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alisema, ndani ya miaka mitano, sekta hizo mbili zimeonyesha ushahidi wa wazi wa kuimarika kwa msingi wa uchumi wa kijani nchini.

Aliongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, uzalishaji wa mbao kutoka mashamba ya miti ya Serikali unaolimwa kibiashara umeongezeka kutoka mita za ujazo 1,108,791 hadi 1,264,535, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 155,000 m³.

Aidha, viwanda vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya misitu vimeongezeka kutoka 636 mwaka 2020 hadi 1,671 mwaka 2025, huku viwanda vidogo vidogo kama vya useremala vikifikia zaidi ya 7,000 kote nchini.

Waziri Chana alisema, thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi nayo imepanda kwa kasi, kufikia Shilingi 458.47 Bilioni mwaka 2024/2025, kutoka Shilingi 105.68 Bilioni mwaka 2020/2021. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 333.8, jambo alilolieleza kuwa ni matokeo ya kuimarika kwa viwango vya usimamizi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

Katika upande wa nyuki, Serikali imewezesha ujenzi wa viwanda nane (8) vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, kutoka kiwanda kimoja (1) mwaka 2020. Viwanda hivyo vimejengwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Iringa, Katavi na Geita.

Mpaka kufikia Aprili 2025, Tanzania imeuza nje ya nchi jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya Shilingi 15.86 Bilioni, ikilinganishwa na tani 430.61 za mwaka 2020/2021 zenye thamani ya Shilingi 5.17 Bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 206.9.

Kutokana na mafanikio haya, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika mwaka 2027 na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya mazao ya misitu na nyuki ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Tunajenga msingi wa uchumi wa kijani unaozingatia uhifadhi, maendeleo ya viwanda na ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza Waziri Chana.

Katika hatua nyingine, Waziri Chana amewakaribisha wabunge wote na wadau wengine wa sekta ya maliasili kushiriki maonesho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yanaendelea jijini Dodoma, na kufikia kilele chake kesho Mei 20, 2025 katika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here