Ziara ya Samia Ruvuma na Galileo katika kisa cha “Eppur si Muove”

0

Na Mwamba wa Kaskazini

LEO Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake katika mkoa wa Ruvuma na kuacha mijadala mingi nyuma ya ziara hiyo.

Wapo, na hasa wapinzani, wanaojadili baadhi ya kauli kutoka kwenye ziara hiyo (ni kawaida yao) lakini wapo wanaoijadili ziara hiyo kama moja ya ziara zenye mafanikio adhimu katika medani za siasa nchini.

Katika tafakuri yangu leo juu ya ziara hii imenijia kauli ya mwanafalsafa wa kale kabisa Galileo Galilei (1564–1642) ambaye mwaka 1633 akiwa anatishiwa kuuawa kwa kosa la “uzushi” kwa wakati huo aliposema dunia inazunguka jua na kutakiwa kukanusha uzushi huo alikomaa na kusisitiza: “eppur si muove.”Nitafafanua.

Turudi Ruvuma. Kwa maoni yangu ziara hii ya Dkt. Samia Ruvuma imekuwa na mafanikio muhimu kisiasa na wachambuzi wa sayansi na sanaa za siasa (the art and science of politics) wamehitimisha kwa haya:

               #Amesikiliza

Katika sayansi za siasa moja ya sifa kubwa ya kiongozi wa kimageuzi ni uwezo wa kwenda kusikiliza wananchi wake. Ziarani Ruvuma Dkt. Samia ameonekana akitulia tuli kuwasikiliza wabunge, kusoma mabango ya wananchi na kujua wanataka nini.

Hili amefanikiwa na ni pigo kwa wengine kwani wakati yeye anasikiliza (wananchi) wapinzani wao wanasikilizia hawajui wasimame wala waje na ajenda gani,maana wanashika hili wanaacha, wanavamia lile wanasahau hili!

        #AmepataMrejesho

Mafanikio mengine ya ziara hii ni Rais kupata mrejesho wa moja kwa moja wa mikakati yake ikiwemo falsafa yake ya 4R.

Nimemuona Rais Samia kule Namtumbo, Mbinga na kwingineko akisoma mabango, akiwahoji wananchi na zaidi akisikiliza mtazamo wa wawakilishi wa wananchi wakimuonesha wapi sera zake zinakwenda salama na wapi kuna shida pafanyiwe kazi zaidi.

Haya yanamtokea wakati wapinzani wake kisiasa mrejesho pekee kwa sasa wanaoujadili ni hasara waliyoingia na kuchapisha mabango na hayakupata nafasi katika maandamano yaliyoshindwa kabla ya kuanza!

              #AmetiwaMoyo

Ziara hii anasema Profesa mmoja wa siasa UDSM alipohojiwa akisema “naitazama pia ziara hii kuwa ni ya kumtia moyo Rais Samia ambaye Serikali yake inaleta mageuzi mengi na imemwaga mabilioni ya pesa kusukuma miradi ya kuboresha maisha ya wananchi kila kona ya nchi.”

Nakubaliana naye. Ziara hii tumemuona Dkt. Samia akiwauliza wananchi umeme? wanajibu upo! Bei nzuri ya mahindi? Tumepataa! Maji? Yapooo ila tunataka zaidi!! Nakadhalika. Hili ni jambo kubwa kwa Rais au mgombea yeyote wa uongozi hasa siasa za mwaka 2025.

Naweza kusema hakuna yeyote anayefikiria Urais mwakani anayepata fursa hii adhimu kama Dkt. Samia. Yeye anapiga kazi, wengine wanapiga soga!

       Kuteta Vs Kutekeleza

Ziara hii pia inaleta ufafanuzi wa kwa nini watabiri wa mambo ya siasa wanaiona 2025 ni mwaka wa ushindi mkubwa wa Dkt. Samia katika uchaguzi na anaweza kuweka historia mpya ya idadi ya kura za Urais!

Unashangaa. Sio mimi ni wanasayansi na sanaa za siasa! “Siri ni hii: ukiangalia wiki nzima hii wakati Dkt. Samia yeye yuko na wananchi, wapinzani wake walikuwa twitter wakihamasisha maandano, wakijibizana na wananchi na/au wanasukuma ajenda wanazopewa na wakoloni mamboleo,” anasema mchambuzi wa siasa Dkt. Laban Luteiko wa Kituo cha Diplomasia ya Umma (Public Diplomacy Center for Africa) chenye makazi yake jijini Nairobi.

Ni kwa sababu hii makala haya katika kuonya watu wasilalamike katika yajayo imeazima neno la kitaliano cha zamani “eppur si mouve” kutoka kwa Galileo Galilei kwamba: (hata mkiniua) lakini nasisitiza dunia inazunguka jua.”

Basi nami vivyo hivyo nahitimisha kwa ziara hii ya Ruvuma na staili ya utendaji wake Rais Samia ya kushuka chini kwenda kusikiliza, kujionea, kupata mrejesho na kisha kuongeza nguvu ya utekelezaji, huku wapinzani wake wakibaki watu wa matusi na uzushi mitandaoni, basi hata nami mkinitisha au kuniwekea mtutu wa bunduki nitasisitiza tu kuwa “Samia si Muove” (Naiona Tanzania 2025 inakwenda na Samia).

Katavi walithibitisha “eppur si muove” wakaja Morogoro sasa Ruvuma nao wametoa kali zaidi kwa kuthibitisha si tu “Uppur si muove” bali sasa ni “Samia si Muove” kwamba sasa Watanzania wanaenda na Samia.

Nasema “Samia si muove” na alluta continua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here