KAIMU Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Roina Ilomo, amewataka wenyeviti wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mlandizi kufanya kazi kwa uadilifu, akisisitiza kuwa baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kutokana na uuzaji holela wa viwanja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo Mlandizi, Ilomo alisema kuwa asilimia kubwa ya migogoro ya ardhi inayowasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya inahusisha vitendo vya baadhi ya wenyeviti wasio waaminifu.
“Migogoro mingi ya ardhi inayoletwa kwa Mkuu wa Wilaya, asilimia kubwa wenyeviti wa maeneo husika wanahusika moja kwa moja. Ni lazima tufuate maadili na sheria ili kuzuia malalamiko ya wananchi,” alisisitiza Ilomo.
Mbali na hilo, aliwataka viongozi hao kushughulikia changamoto za wananchi kwa ufanisi na kuepuka kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Alisema, masuala yanayozidi uwezo wao yanapaswa kuelekezwa katika mamlaka husika kwa ufumbuzi wa haraka.
Katika uzinduzi huo, John Pili alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mlandizi, huku Geofrey Kazinduki akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.