WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari Mpya ya Kisiwa Mgao, mkoani Mtwara, ambao umefikia asilimia 25 ya utekelezaji wake.
Akizungumza baada ya ziara yake ya kutembelea na kukagua mradi huo, Disemba 20, 2025, Waziri Prof. Mbarawa ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji pamoja na ubora wa kazi zinazoendelea kufanyika katika eneo la mradi.
Waziri Prof. Mbarawa amesema, Bandari mpya ya Kisiwa Mgao ni mradi wa kimkakati unaolenga kuimarisha sekta ya uchukuzi wa majini na kukuza uchumi wa Taifa, hususan kwa ukanda wa Kusini, hivyo ni wajibu wa TPA na wadau wote kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia ubora, uwazi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Aidha, Waziri Mbarawa alibainisha kuwa kukamilika kwa Bandari ya Kisiwa Mgao kutaongeza uwezo wa nchi katika kuhudumia shehena ya mzigo mchafu, kupunguza msongamano wa shughuli za bandari ya Mtwara, na kuimarisha biashara pamoja na usafirishaji wa bidhaa katika ukanda wa Kusini na nchi jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema mradi huo utakuwa chachu kubwa ya maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa wa Mtwara na maeneo ya jirani kwa kuongeza fursa za ajira, kuchochea shughuli za kibiashara, na kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa za kimkakati, hususan makaa ya mawe, saruji na mbolea.
Mbossa aliongeza kuwa kukamilika kwa bandari hiyo mpya kutaongeza mapato ya Serikali na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi ya ushindani wa kikanda katika sekta ya bandari na usafirishaji wa majini.
Ziara ya Waziri Prof. Mbarawa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inatekelezwa kwa ufanisi, uwajibikaji na kwa kuzingatia malengo ya kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha ustawi wa wananchi.