KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekta ya Miundombinu katika Sekretarieti za Mikoa kusimamia miradi kikamilifu kwa mujibu wa mikataba ili kuhakikisha zinakuwa na ubora.
Mhandisi Mativila ametoa maelekezo hayo leo Februari 5, 2025 kwenye kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma, kilicholenga kujadili utekelezaji wa miradi ya ujenzi, ukarabati, na matengenezo ya miundombinu katika Mikoa 26, Wilaya 139, na Halmashauri 184 nchini.
“Ubora wa kazi ni jambo la msingi. Kama ni jengo, lijengwe kwa viwango vinavyostahili. Kuna baadhi ya majengo yanapotembelewa na waheshimiwa wabunge, hubainika kuwa hayana ubora,” alisisitiza Mhandisi Mativila.
Aidha, amewataka viongozi hao kuwa na mipango thabiti ya muda mfupi, muda wa kati, na muda mrefu ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kama ilivyokusudiwa na serikali.
Mhandisi Mativila amewasihi kuboresha utendaji wao kwa lengo la kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa watanzania wa mijini na vijijini.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi wa Miundombinu wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Ezron Kilamhama, ameahidi kushirikiana na wahandisi wa halmashauri kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa mujibu wa mikataba na kwa viwango vinavyostahili.
Msanifu Majengo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Chabu Nghoma, alisema wataandaa mpango kazi wa utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na kuuwasilisha kwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI ndani ya mwezi wa pili kwa ajili ya tathmini.
Ofisi ya Rais – TAMISEMI ina jukumu la kuratibu matengenezo, ukarabati, na ujenzi wa miundombinu ya barabara, majengo, na miundombinu mingine katika ngazi za mikoa, Wilaya, na Mamlaka za Serikali za Mitaa.