Na Abdulrahim Khamis OMPR
WANANCHI wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa Jirani wametakiwa kushiriki katika Hafla ya Uzinduzi wa Matokeo ya Awali ya Sensa ya Watu na Makazi hafla inayotarajiwa kufanyika Oktoba 31, Mwaka huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Hemed Suleiman Abdulla ametoa Wito huo wakati akizungumza na Vyombo vya Habari baada ya ukaguzi na kupokea Taarifa ya Maandalizi ya Hafla ya Uzinduzi wa Matokeo ya Awali ya Sensa ya Watu na Makazi katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Alisema, Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi la Mwezi Agosti Mwaka huu limekamilika kwa Asilimia kubwa ambapo kwa sasa Wananchi wana hamu ya kujua Matokeo ya Sensa hiyo yenye faida kubwa kwa maendeleo ya Tanzania.
Mwenyekiti Mwenza huyo ambaye Pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema, zoezi la Uzinduzi wa Matokeo hayo litafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Kiwanja cha Jamhuri Jijini Dodoma ambapo amewataka Wananchi kushiriki kikamilifu katika Uzinduzi huo.
Aidha, Hemed amewapongeza Wananchi kwa Ujumla kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kipindi chote cha Zoezi hilo na kueleza kuwa Serikali inathamini mashirikiano yao hayo.
Sambamba na hayo Hemed ameridhishwa na Maandalizi mazuri ya Hafla hiyo ya uzinduzi na ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa mstari wa mbele katika Maandalizi hayo.
Naye, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma ameeleza kuwa Maandalizi ya Hafla ya uzinduzi huo yamekamilika kwa Asilimia kubwa ambapo Serikali itakuwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kukamilisha Maandalizi hayo.
Aidha, Hamza alisema Serikali imezingatia Ushiriki wa Wananchi wa Pande zote mbili za Muungano Bara na Visiwani ambapo Wananchi mbali mbali wanatarajiwa kushuhudia Uzinduzi huo.