BARAZA la Taifa la Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi (NEEC) limesema, hadisasa watu 90,000 wamesajiliwa kwenye Kanzidata ya programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA).
Hayo yamesemwa leo Oktoba 22, 2024 na Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ushiriki wa Watanzania, Neema Mwakatobe kwenye mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo alisema, programu ya IMASA inatekelezwa kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Mikoa Mitano ya Zanzibar ambapo hivisasa wamefika kwenye mikoa 24 na utekelezaji wa programu hiyo unatarajiwa kuanza rasmi mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema, kwenye mikoa ambayo wameitembelea, wamezungumza na Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Makatibu Tawala na watendaji wengine na kujadiliana kuhusiana na fursa ambazo zinapatikana kwenye mikoa hiyo.
“Tumejadiliana na viongozi wa mikoa kuhusu shughuli za kiuchumi zinazopatikana kwenye maeneo yao ambazo zitawanufaisha wananchi. Huko tunaibua vipaumbele ambavyo vitagusa makundi mbalimbali; akinamama, vijana na walemavu, ” alisema Neema.
Alisema, baada ya kukamilika kwa Awamu ya Kwanza, wataingia kwenye Awamu ya Pili ambayo itahusisha upelekaji wa fursa na programu mbalimbali kulingana na shughuli za kiuchumi walizoziona kwenye mikoa waliyopita. “Programu hii ya IMASA inazitambua Programu nyingine zilizopo nchini ikiwemo BBT.”