WAKAGUZI wa hesabu za Serikali wametakiwa kuutumia kikamilifu mfumo ulioboreshwa wa uhifadhi wa mali za umma, ili kuimarisha uwazi, ufanisi na usahihi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo katika ukumbi wa Afisi ya Msajili wa Hazina, Maisara – Zanzibar, Afisa Mdhamini wa Ofisi hiyo, Awatif Fauz Abdulrahman, alisema mfumo huo utaongeza ufanisi katika kufunga hesabu za mwaka kwa wakati na kutoa taarifa sahihi za mali za Serikali.
“Mfumo huu utawasaidia wahasibu na wakaguzi wa ndani kurikodi na kufuatilia mali za Serikali kwa uhalisia wake. Utaimarisha utoaji wa taarifa sahihi za mali zinazoingia na kutoka katika taasisi za umma,” alisema Awatif.
Ameongeza kuwa mfumo huo umeundwa kusaidia taasisi za umma katika upokeaji, uhifadhi na utoaji wa taarifa za mali za Serikali, hatua itakayochangia kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha, alisema ofisi yake imeandaa mafunzo kwa taasisi zote za Serikali ili kuhakikisha watendaji wanapata uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mfumo huo, na hivyo kuepuka changamoto wakati wa utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Suleiman Juma Is-hak, Mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema mfumo huo umeboreshwa kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa mali za umma na kurahisisha ukusanyaji wa taarifa kutoka taasisi zote za Serikali.
“Mfumo huu utaiwezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina kusimamia mali za umma kwa ufanisi zaidi, kwani utakuwa unatumika kwa pamoja na taasisi zote za Serikali,” alisema Suleiman.
Naye Biubwa Hassan Fadhili, Mkaguzi wa Mifumo kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, alisema mfumo mpya umeboreshwa zaidi ikilinganishwa na ule wa awali, kwani sasa una hatua za uthibitisho katika kila ngazi ya uingizaji wa taarifa.
Mafunzo hayo yamehusisha watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, wakaguzi wa ndani na nje, pamoja na maafisa wa e-Government, yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo mpya wa uhifadhi wa mali za Serikali.