‘Vijiji vyote Tanzania bara kufikiwa na umeme’

0
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza
Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Ameeleza hayo bungeni, jijini Dodoma Septemba 6, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe ambaye alitaka kujua ni  lini Serikali itapeleka umeme kwenye Vijiji vya Namikunda, Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na
Kata ya Temeke.

Akijibu swali hilo, Kapinga alisema katika Jimbo la Masasi, Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo havikuwa na umeme ambapo hadi kufikia Agosti 15, 2023, vijiji 11 vimeshawashwa umeme na vijiji 6 vitakamilika kabla ya mkataba wa Mkandarasi kuisha Desemba 31, 2023.

Aliongeza kuwa, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na Chakama vimekwishawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia Desemba 31, 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa umeme.

Alisema, kwa sasa, zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya Temeke (Mkarango) bado linaendelea na nguzo tayari zimekwisha simamishwa katika kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here