WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Vijana wana nafasi ya kipekee na ya kimkakati katika kuutetea, kuuenzi na kuukuza Muungano kwa vitendo, kauli na maamuzi yao katika maeneo mbalimbali wanashiriki katika mijadala chanya kuhusu Muungano.
Ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Muungano na Maonesho ya Ubunifu kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Zanzibar yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Aprili 24, 2026 ambayo kaulimbiu ilikuwa Kuunganisha Ubunifu na Fursa.
Masauni amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si tu historia ya kisiasa, bali ni rasilimali ya maendeleo. Ndani yake kuna fursa nyingi zinazoweza kuendelezwa kupitia fikra bunifu za vijana, hasa ninyi mlio katika vyuo vikuu, ambao ni hazina ya maarifa, utafiti na uvumbuzi.
“Katika nyanja mbalimbali kama uchumi wa buluu, teknolojia ya kidigitali, kilimo cha kisasa, utalii, na biashara, Muungano umefungua milango ya ushirikiano mpana kati ya pande mbili. Ushirikiano huu unahitaji ubunifu wa vijana ili kubadilisha fursa hizi kuwa ajira, biashara na suluhisho endelevu.
“Katika kutekeleza suala hilo kwa vitendo, Ofisi ya Makamu wa Rais iliona haja na umuhimu wa utolewaji wa elimu ya Muungano kwa kuandaa Mpango Kabambe wa Utolewaji wa Elimu kwa umma kuhusu muungano kwa makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo kundi la Wanafunzi wa Vyuo vikuu ambao wengi wao wamezaliwa baada ya Muungano.
Masauni amesema Vijana wana wajibu wa kuelimika na kujielimisha kuhusu Muungano; kujifunza historia, misingi na faida za Muungano; Kushiriki katika programu za elimu ya Muungano mashuleni na vyuoni; kutafuta taarifa sahihi; na kuwa na uwezo wa kuchanganua masuala ya Muungano.
Amesisitiza kuwa Vijana wana wajibu wa kuchuja taarifa wanazokutana nazo mtandaoni; Kupinga habari za uongo au propaganda zinazodhoofisha Muungano; na Kushiriki katika kampeni za ‘’fact – checking’’ na uelimishaji wa wenzao.
Vijana wanaweza Kutengeneza maudhui ya kidigitali kuhusu Muungano (video, blogs, podcasts); Kutumia mitandao ya kijamii kueneza ujumbe wa umoja; na Kuanzisha majukwaa ya kidigitali ya majadiliano ya Muungano.