◼️Wazalisha faida ya Milioni 76 mavuno ya kwanza
VIJANA wanaonufaika na mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) waliopo Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Nyegezi jijini Mwanza wameanza kupata matunda ya mradi huo kwa kupata faida ya takribani Shilingi Milioni 76 baada ya kuvuna samaki katika Vizimba 3 Novemba 18,2026.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka mara baada ya kuongoza hafla ya uvunaji wa samaki kwenye vizimba hivyo ambapo amesema kuwa mradi huo umekuwa na matokeo chanya ukilinganisha na miradi mingine ya kisekta iliyowahi kufanyika awali.
“Kwa maneno mengine ni kwamba vizimba vyote vilivyopo hapa vikivunwa kwa wakati mmoja ni zaidi ya Bilioni 2 zitapatikana lakini ili kuhakikisha soko linaenda vizuri tumeamua kuvuna kwa awamu ili kuhakikisha bidhaa haizidi wanunuzi,” amesema Nanauka.
Aidha, Nanauka amesema kuwa vijana hao wamewekewa mfumo endelevu ambapo watarejesha mkopo wao kwa awamu huku benki ya Maendeleo ya Kilimo ikiwapa asilimia 85 ya uwekezaji unaofuata baada ya kukamilika kwa mradi wa kwanza jambo litakalowahakikishia kufanya uwekezaji mwingine wakati wakiendelea na uliopo.
Kwa upande wake mratibu wa Mradi huo kutoka FETA Peter Masumbuko amesema kuwa vizimba hivyo vina uwezo wa kubeba tani tatu za samaki kwa kila kizimba na hivyo kufanya uzalishaji wa jumla wa vizimba vyote kufikia takribani tani 240.
Naye mwakilishi wa vijana hao Erasto Deo mbali na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha mtaji wa kutekeleza mradi huo amesema kuwa mavuno waliyopata yanawahakikishia kubadili maisha yao kiuchumi ambapo amekiri kiasi cha pesa walichopata hawakuwahi kufikiria kukipata hapo awali.
Jumla ya Vijana 167 waliopo katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara wamenufaika na mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) ambapo idadi hiyo inatarajiwa kufikia vijana 252 mara baada ya uzinduzi wa mradi huo utakaofanyika Wilaya ya Chato mkoani Geita Novemba 20,2026.