JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imepokea tuzo ya UN AI for Climate Action Award 2026, inayotolewa kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa unaotambua ubunifu wa matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Tuzo hiyo imekabidhiwa pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika Antalya, nchini Uturuki.
Akizungumza katika hafla ya kupokea tuzo hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amempongeza Dkt. Upendo Ernest Lyimo kwa ubunifu na mchango wake ulioiwezesha Tanzania kupata utambuzi huo wa kimataifa.
Tuzo hiyo inatokana na ubunifu wa CLIMAID, mfumo wa kidijitali uliobuniwa na Dkt. Upendo Ernest Lyimo unaotumia Akili Unde, taarifa za satelaiti, takwimu za hali ya hewa na taarifa za kijamii kuchambua na kutabiri hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mfumo wa CLIMAID unasaidia, Kutambua maeneo yaliyo katika hatari ya ukame,
Kuwezesha utoaji wa tahadhari za mapema. Kutathmini athari na hasara za kiuchumi na zisizo za kiuchumi pamoja na kushauri hatua za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akielezea dhamira yake, Dkt. Upendo Ernest Lyimo amesema lengo lake ni kuhakikisha kuwa taarifa za kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha kuwa hazibaki kwenye tafiti na ripoti pekee, bali zinatumika kuchukua hatua zinazolinda maisha, uchumi na mazingira.
Aidha, Masauni amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua mafanikio hayo na kuunga mkono juhudi za kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikishana uzoefu na kukuza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika kuendeleza suluhisho za kiteknolojia dhidi ya changamoto za tabianchi.