KATIKA hafla ya makabidhiano ya vifaa vya TEHAMA, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema vifaa vilivyokabidhiwa kwa Shirika la Posta Tanzania vina thamani ya takribani Shilingi Milioni 288.
Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta za mezani (desktop) 30, UPS 30, kompyuta mpakato (laptops) 7, Personal Digital Assistants (PDAs) 50, mashine za kopia zenye uwezo mkubwa (Heavy-Duty Photocopy Machines), pamoja na vifaa vya ukarabati wa miundombinu ya mtandao (LAN materials).
Aidha, Mhandisi Mwasalyanda amefafanua kwamba, katika mwaka wa fedha 2023/24, UCSAF ilinunua na kukabidhi vifaa saidizi vya TEHAMA (PDAs) 250, vilivyosaidia kuboresha utoaji wa huduma za posta, ikiwemo ufuatiliaji wa vifurushi, barua, na uwasilishaji wa taarifa kupitia mtandao wa Shirika la Posta.
“Dunia ya leo inakimbia kwa kasi kwenye nyanja za teknolojia, na kama taifa hatuna budi kuendelea kukabiliana na mabadiliko haya. Makabidhiano haya ni hatua mojawapo ya kuhakikisha Shirika la Posta linaendana na nyakati,” aliongeza Mhandisi Mwasalyanda.