Na Fauzia Mussa, MAELEZO
JUMLA ya wagonjwa 4,579 wa ugonjwa wa macho (red eyes) wameripotiwa katika vituo vya afya, na hospitali Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya ugonjwa huo huko Wizara ya Afya wilaya ya mjini Naibu Waziri wa Wizara hiyo Hassan Khamis Hafidh amesema idadi ya takwimu hizo zimejumuisha wagonjwa waliofika kwenye vituo vya afya na hospitali za binafsi na serikali Unguja na Pemba.
Aidha, amewataka wananchi kuacha kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza sambamba na kuchukua tahadhari za usafi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara ili kujikinga na maradhi hayo .
Alisema, endapo jamii itaendelea kutumia dawa hizo kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hilo hivyo aliwataka wananchi kufika hospitali mara tu wanapoona dalili za ugonjwa huo ili kupata matibabu stahiki na kwa wakati sahihi.
Hata hivyo, aliiasa jamii kuacha kushikana mikono na mtu mwenye maambukizi au kugusa sehemu ya kitu ambacho kimeguswa na mtu huyo, na kuwataka kutumia maji baridi kunawia uso mara kwa mara, pamoja na kujitenga wakati wa kusubiri huduma katika vituo vya afya ili kuepusha maambukizi mapya.
“Ni vizuri mgojwa yeyote wa macho asisubiri eneo walilokaa wagonjwa wengine atibiwe chumba maalum kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa namna hiyo na akimaliza matibabu aende moja kwa moja nyumbani ili kupunguza hatari ya maambukizi mapya” alisema Naibu Waziri.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ugonjwa huo mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho Dkt. Rajab Mohammed Hilal alisema, ugonjwa wa macho mekundu husababishwa na virusi wanaoitwa Adenovirus na kupelekea maambukizi ya kirusi kwenye ngozi nyembamba inayozunguka gololi la jicho (conjunctiva) pamoja na kioo (Cornea) cha jicho.
Aliongeza kwa kusema, ugonjwa huo unaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja mwenye ugonjwa huo na kwenda kwa mwengine na kusambaza maambukizi kwa haraka sana ndani ya siku 10 hadi 12.
Alifahamisha kuwa dalili kubwa za ugonjwa huo ni pamoja na jicho kuwa jekundu, kuwasha na kuchomachoma, mifuniko ya macho kuvimba, macho kuogopa mwangaza, macho kutoa matongo matongo meupe au ya njano kuona ukungu kwa uoni wa mbali katika macho, pamoja na maumivu ya macho.
Alisema, miongoni mwa athari za muda mrefu zinazoweza kujitokeza endapo jamii itaendelea kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ni pamoja kupunguza uoni.
Itakumbukwa kuwa wiki mbili zilizopita ugonjwa wa macho mekundu (red eye) uliripotiwa katika mikoa ya Tanzania bara na kutokana na maingiliano ya wananchi ya mara kwa mara ugonjwa huo umeweza kuingia Visiwani Zanzibar.