‘Tuwe na utamaduni wa kusameheana kwa kila jambo’

0

WAUMINI wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuwa na utamaduni wa kusameheana kwa kila jambo ambalo wamekoseana baina yao ili kuweza kupata radhi za Allah (S.W) na kupata makazi mema kesho akhera.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid ABRAWY uliopo Fuoni Mambo Sasa mara baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Alisema, suala la kusameheana kwa waumini pamoja na wanchi kwa ujumla ndio jambo pekee ambalo linamfanya mwanadamu kupata radhi kutoka kwa Allah (S.W) hasa katika kipindi hichi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan, mwezi ambao una mafundisho mengi ndani yake.

Alhajj Hemed alisema, Ramadhani ni Chuo chenye kuwafundisha waumini mambo mbali mbali ambayo Mwenyezi Mungu huyaridhia kutoka kwa waja wake ikiwemo ibada hivyo ni vyema waumini kudumisha ibada za faradhi na sunna ili kupata Maghfira kutoka kwa Mwenyezi mungu.

Aidha, Alhajj Hemed amewasisitiza wazazi na walezi kuwawekea mazingira mazuri vijana wao katika kufuata maadili mema sambamba na kuwakurubihisha katika ibada hasa kipindi hichi cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kuweza kuendeleza ibada hata kwenye miezi mengine.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema, vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, hivyo ni lazima kila mzazi na mlezi kujitathmini katika malezi kwa vijana wao wanaowalea kwani kufanya hivyo kutasaidia kupata wanazuoni watakaoweza kuisimamia nchi pamoja na dini kwa ujumla. 

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kuzidi kuwaombea dua viongozi wao hasa katika kumi hili la Maghfira ili kuiacha nchi yenye neema kwa faida ya vizazi vya sasa na vya baadae.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Sheh HASSAN HEMED ABDALLA amewataka waumini wa Dini ya Kiislam kufanya yale yote aliyoyafanya Mtume muhamad (S.A.W) ikiwemo kufanya ibada kwa wingi za faradhi na za Sunna, kusaidiana, na kutoa sadaka ili kupata fadhila za kumi hili la maghfira.

Alisema, waislamu ni lazima kufanya matendo mema tena kwa taqwa huku wakitarajia kupata fadhila kutoka wa mwenyezi mungu (S.W) kwa kila jambo hasa kwenye mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here