Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi, amevitaka vyama vya siasa kutokubali kufarakanishwa na genge la watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya utekaji nchini na kuwapa ushindi.
Dkt. Nchimbi alisema hayo leo (Septemba 13, 2024) kwenye Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Alisema, hivi karibuni Kiongozi wa Chadema (Ally Kibao) alitekwa na kuuawa kikatili, jambo hilo sio dogo, ndio maana wameona walizungumzie ikizingatiwa Ilani ya CCM ukurasa wa 156 inasema, moja ya mambo ambayo watayafanya ni kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendelea kudhibiti usalama wa Raia na mali zao.
“Mtu yoyote anayeshiriki kuteka raia au mauaji ya raia, ni wazi wanajua wanafanya hivyo ili kuharibu taswira ya CCM mbele ya Umma na ndio maana kama ni mtu au genge la watu linajihushisha na kuteka watu au kuua watu haliwezi kuwa na nia njema na CCM,” alisema Dkt. Nchimbi.
Aliendelea kusema: “Ni Mwendawazimu pekee yake anaweza kutamka kwamba CCM inaweza ikafanya jambo la kujiumiza yenyewe, CCM sio chama cha watu wajinga, ni chama cha Siasa kisichojitambua ndicho kinaweza kufanya matendo ya kufanya kikosane na wananchi wake,”
“Watu wenye nia mbaya ndio wanaoendesha magenge ya uhalifu nchini ili kukikosanisha chama chetu na wananchi na kufarakanisha Taifa, ni watu hawa wanasababisha watu wenye busara sana waongee maneno yasiyotarajiwa,”
Dkt. Nchimbi alisema amemsikia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema Freeman Mbowe akitoa muda wa mwisho wa Serikali kuwataja wahusika wa matendo hayo maovu na akisema ikifika Septemba 23,2024 iwapo hawajatajwa watachukua hatua.
“Kwa mtu kama Mbowe, mwenye hekima kubwa, akiwa amefikishwa hapo na genge la watekaji; naye kaamini, kwamba kiongozi unaweza kumpa rais muda wa mwisho, ukishafikishwa hapo, ujue genge la watekaji limefanikiwa sana,” alisema Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi alisema, kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha kwamba, genge hilo halifanikiwi kwenye mkakati wake wa kufarakanisha watanzania na kuwapa ushindi.
“Ni wajibu wetu sisi na vyama vya upinzani, kuhakikisha tunashirikiana kuhakikisha genge la watekaji halifanikiwi kwenye mkakati wa kutufarakanisha. Kosa kubwa kuliko lote, ni kuwapa ushindi genge la watekaji,” alisema Dkt. Nchimbi.
Nchimbi alitolea mfano tukio lililotokea nchini Marekani, ambapo Donald Trump ambaye ni Rais Mstaafu wa nchi hiyo na mgombea urais kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika Novemba, mwaka huu, alipigwa risasi kwenye jaribio la kutaka kumuua, lakini tukio hilo halikusabababisha mgawanyiko ndani ya Taifa hilo.
“Kilichojitokeza, vyama vikuu vya upinzani vinavyojitambua, chama chake cha Republican kililaani vikali na kikataka hatua zichukuliwe, chama cha Democrat kililaani vikali na kikataka hatua zichukuliwe,”
“Hatujasikia Democrat wanawalaumu Republican, wala hatujasikia Republican wanawalaumu Democrat, kwasababu wamejua lengo la anayefanya madhara yale ni kuwafarakanisha kama Taifa, wamekataa kufarakanishwa,” alisema Dkt. Nchimbi.
Alisema, Chama cha Mapinduzi kinavitaka vyama vya upinzani kuiga jambo hilo na kukataa kufarakanishwa “sisi kama chama, tumefanya kila njia kukataa kujiingiza kwenye mijadala ambayo haina tija,”
Dkt. Nchimbi alisema, amesikia kauli za vijana wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) na kauli mbiu yao mpya inayosema ‘SAMIA MUST GO,’ jambo ambalo haliwezekani, ikizingatiwa Rais Samia Suluhu Hassan, yupo kwenye nafasi hiyo Kikatiba na atamaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba.
“Moja ya sifa ya kijana anayeandaliwa vizuri, anapaswa kufundishwa kuheshimu Katiba, tunaweka uchaguzi miaka mitano mitano ili wale watakaokuwa hawaridhiki ndani ya hiyo miaka mitano wapate nafasi nyingine ya kuchagua,” alisema.
Aliongeza, haiwezekani katikati ya msimu kukazuka kauli za kutaka Rais aachie ngazi “kwa wanaojua demokrasia, ndio maana Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema mpaka leo, kila zilipoanza kelele ndani ya Chadema kwamba ‘Mbowe Must Go,’ zilishindikana kwa sababu ni kinyume cha Katiba yao.”
Alisema, wanaolinda Katiba ya Chadema wanamlinda kwa nguvu zao zote na imeshatokea zaidi ya mara tatu Mbowe akitakiwa aachie Uenyekiti wa chama hicho, lakini bado yupo kwenye nafasi yake.
“Mbowe hajaenda popote na Samia atakuwepo,” alisisitiza Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchini.