Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WATANZANIA wametakiwa kuepuka kubebeshwa chuki kwa kuuchukia upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano na badala yake wanapaswa kuijenga Tanzania, na kushirikiana na kiongozi yeyote anayechaguliwa bila kujali anapotoka.
Katibuwa Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari visiwani hapa na kukemea kitendo cha baadhi ya watu wanaotaka kuwagawa watanzania ambao wameishi kwa umoja kwa miaka mingi.
Mbeto alisema, mwaka 1964 waasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, waliunganisha nchi mbili zikawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukubaliana kuwa na mifumo miwili ya kuendesha Serikali.
“Kwamba, tutakuwa na Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Muungano wetu tukakubaliana suala la uraia litakuwa la Jamhuri ya Muungano, kwa maana haitakuja kutokea kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atatoka nje ya upande mmoja wa Jamhuri yetu,” alisema.
Aliendelea kusema “Ni jambo la kushangaza sana kuna baadhi ya viongozi na baadhi ya wananchi kuchukulia kwamba akitoka Rais wa Jamhuri ya Muungano sehemu moja sio halali, sio kweli. Sisi tukimtafuta rais hatumtafuti kwa kuwa ametoka Zanzibar au Tanganyika.”
Alisema, kwa muda mrefu tumekuwa na Marais mfululizo kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, lakini wala hatujasikia Wazanzibar au sehemu nyingine wakilalamika, kwani wanajua kufanya hivyo ni kuharibu tunu za Taifa.
“Tumekuwa na Mwalimu Nyerere katoka Bara, akaja Mzee Mwinyi katoka Zanzibar, akafuatiwa na Mzee Mkapa anatoka bara, akafuatiwa na Jakaya katoka bara, Magufuli katoka Bara. Rais Samia amekuja baada ya kifo cha Magufuli, ukiona watu wanapandikiza chuki kwa watanzania kuona sehemu moja ya nchi haina haki ya kuwa na kiongozi, sio sahihi,” alisema Mbeto.
Akifafanua zaidi alisema, “Tumeungana tukiwa na nchi zetu zote sawa, tumekubaliana mchakato wa kuwapata viongozi wetu utatokana na vigezo na sifa na kwa mujibu wa Katiba ambayo tulikubaliana. Hata Imani zetu, maazimio ya TANUna Afro Shiraz Party wakati tunaunganisha, tulisema binadamu wote ni sawa na kila binadamu anapaswa kuheshimiwa utu wake bila kujali anatoka upande gani, imani yake ya dini au kabila.”
Alisema, makabila hayaongozi Tanzania na tunapotafuta kiongozi hawaangalii kabila lake, dini yake, wala ametoka kwenye eneo gani, bali kinachopimwa ni vigezo ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Niwaombe sana tusikubali kutumika, tukarudi nyuma na kuanza kuulizana makabila. Baba wa Taifa alikemea sana masuala ya ukabila, udini na ukanda,”
Aidha, Mbeto alisema, kwenye historia ya nchi yetu, amewahi kutoka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Salim Ahmed Salim ametoka Zanzibar, na baada ya hapo hakuna mwingine ametoka visiwani humu, lakini Wazanzibar hawajawahi kupiga kelele kwasababu wanajua hicho sio kigezo cha kupata kiongozi.
“Niwaombe watanzania tusijaribu kuitia nchi yetu kwenye majaribu mazito baadae tukaja kulaumiana kwa faida ya watu wachache wanaoiona Tanzania inaimarika na uongozi wake unafanya vizuri,” alisisitiza Mwenezi Mbeto.