MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema ugonjwa wa saratani unaendelea kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma barani Afrika na duniani kote kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa na uhaba wa huduma za uchunguzi na matibabu.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa Kikanda wa kuwajengea uwezo nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi, uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Hemed amesema kuongezeka kwa matukio ya saratani sambamba na upungufu wa huduma za uchunguzi na matibabu katika maeneo mengi barani Afrika kunahitaji kuimarishwa kwa uwezo wa kitaifa, ushirikiano wa kikanda pamoja na matumizi sahihi ya sayansi na teknolojia.
Ameeleza kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki una jukumu muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa Mradi wa RAF 6060 unaolenga kuimarisha uwezo wa nchi wanachama na kuboresha utambuzi na matibabu ya saratani unafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, amesema mpango mkakati wa mradi huo unalenga kusaidia upatikanaji wa rasilimali watu, kuimarisha uwezo wa watendaji pamoja na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika sekta ya tiba.
Makamu wa Pili wa Rais amefahamisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutekeleza Mradi wa Kitaifa wa URT 6033 unaolenga kupanua na kuboresha matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi, pamoja na kuimarisha huduma za Tiba ya Nyuklia na Tiba ya Mionzi (Radiotherapy).
Sambamba na hayo, amewahimiza washiriki wa mkutano huo kushiriki kikamilifu na kwa njia yenye kujenga ili kuhakikisha mkutano huo unaleta matokeo chanya katika kuimarisha mifumo ya afya na huduma bora za matibabu barani Afrika.
Kupitia ushirikiano na IAEA, Hemed amesema maendeleo makubwa yamepatikana ikiwemo upatikanaji wa dawa za nyuklia, huduma za Tiba ya Mionzi, fizikia ya matibabu pamoja na rediopharmacy, hali iliyoongeza ubora na ufanisi wa matibabu ya saratani.