KAIMU Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo ameweka wazi uelekeo wa Sekta ya Madini katika kuchangia Pato la Taifa ili kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 24, 2024 Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo alisema, katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Tume ya Madini imeweka mikakati endelevu ikiwemo kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs) na vitendea kazi (PoS).
Aidha, alisema kwa kushirikisha Mamlaka nyingine za Serikali zinazosimamia na kutumia rasilimali hizi (Halmashauri, Polisi, TARURA na TANROADS), wataongeza makusanyo yatokanayo na rasilimali ya madini ujenzi na madini ya viwandani.
Alisema, mkakati mwingine ni kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususani utoroshaji wa madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia Masoko na vituo vya madini nchini; kuimarisha vituo vya ukaguzi (exit-points) katika maeneo ya mipakani, bandarini pamoja na viwanja vya ndege lengo likiwa ni kupunguza matukio ya utoroshaji wa madini na hivyo kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na mapato stahiki.
“Uboreshaji na Usimamizi thabiti wa Mfumo wa Utoaji wa Leseni za madini, matokeo ni kupunguza migogoro itokanayo na mwingiliano wa maombi ya leseni, kupunguza muda wa utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya leseni zitakazotolewa kwa mwaka hivyo kuhamasisha uwekezaji,” alisema Mhandisi Lwamo.
Alisema, mkakati mwingine ni kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira, ambapo lengo ni kuongeza mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu unaojali mazingira kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
“Tutaimarisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs) na Maabara katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wadau hivyo kuchochea uwekezaji utakaowezesha Serikali kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini,” alisisitiza Mhandisi Lwamo.
Mkakati mwingine ni kuimarisha shughuli za tafiti zinazohusiana na utambuzi wa vyanzo vipya vya mapato yatokanayo na rasilimali za madini ili kuiwezesha Taasisi hiyo kuongeza wigo wa makusanyo yatokanayo na rasilimali madini ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa wachimbaji wa madini na kuongeza mapato, ajira na kuwa Sekta endelevu.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Lwamo alisema, katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani, Tume ya Madini imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa maduhuli.
Alisema, kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini, kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 tulipewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni Moja, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka,” alisema Mhandisi Lwamo.
Aidha, alisema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini iliendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa Madini nchini.
“Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 mauzo ya madini katika Masoko na Vituo vya Ununuzi wa madini yalikua Shilingi bilioni 2,592.02 na mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo hayo ni kiasi cha Shilingi bilioni 180.13 ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2021/2022 ambapo ilikua Shilingi bilioni 2,361.80 na mapato ya Serikali yaliyopatikana ni Shilingi bilioni 164.09 ambapo mapato hayo yalihusisha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini,”
Mhandisi Lwamo alisema, Tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.
Alisema, jumla ya Mipango 1,050 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,036 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 14 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho.
“Aidha Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Makampuni mbalimbali ya Uchimbaji ambapo katika kipindi rejewa Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,356 ambapo kati ya hizo 18,853 ni Watanzania sawa na asilimia 97.40 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.60 ya ajira zote zilizozalishwa,” alisema.
Vilevile, alisema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.
Alisema, Tume ya Madini imekuwa ikitoa leseni za uendeshaji wa shughuli za madini kwa wadau wake kwa kuzingatia Sheria ya Madini Sura 123. Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, katika kipindi cha kuanzia 2021/2022 hadi 2024/2025, Tume ilikusudia kutoa leseni 37,318 hata hivyo hadi kufikia Septemba 30, 2024/2025 Tume ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni 34,348 sawa na asilimia 92.04 kati ya leseni zilizopangwa kutolewa. Leseni hizo zilijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini.
Pia, Tume imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Madini nchini kwa kutoa leseni kubwa kwa makampuni mbalimbali ya uchimbaji wa madini. Leseni hizo za uchimbaji mkubwa wa Madini zilitolewa kwa Faru Graphite Corporation Limited itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya kinywe Wilayani Mahenge yenye leseni SML- 676/2022; Mamba Minerals Corporation Limited inayojihusisha na uchimbaji wa Rare Earth Elements-REE katika eneo la Ngualla yenye leseni SML 693/2022 iliyopo mkoani Songwe.
Leseni nyingine ni ya usafishaji madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera yenye leseni SM- 651/2021; na Sotta Mining Corporation Limited iliyopo Mkoani Mwanza, Wilaya ya Sengerema yenye leseni SML-653/2021.
“Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika Sekta ya Madini pamoja na Sekta fungamanishi nchini ikiwemo Tume kuendelea kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa,” alisema Ramadhani Lwamo.