Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza uhusiano na ushirikiano baina yao kwa kuzingatia udugu wa kihistoria uliopo.
Dkt. Mwinyi alisema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Uganda nchini Tanzania Fred Mwesigye, aliefika kujitambulisha.
Alisema, wananchi wa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki wana udugu wa kihistoria, hivyo ni vyema kuwepo utaratibu wa kutembeleana na kushirikiana katika mambo mbali mbali.
Alieleza kuwa, Zanzibar ni kisiwa ambapo Sekta ya Utalii imepewa kipaumbele na kusema kuna maeneo mbali mbali ya kushirikiana.
Aidha, alisema kuna umuhimu wa kuendeleza mashirikiano ya kibiashara kati ya Uganda na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwa viongozi kufanya mazungumzo ili kuwawezesha wafanyabaishara wa nchi mbili hizo kuendeleza biashara zao.
Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa mwaliko aliotuma kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu wa kuzuru nchi hiyo hapo baadae, ambapo Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kumwakilisha.
“Naomba unifikishie salamu zangu za dhati kwa Rais Museveni…tunafahamiana kwa kipindi kirefu sasa”, alisema.
Nae, Balozi wa Uganda nchini Tanzania Fred Mwesigye alisema, nchi hiyo inahitaji walimu wa kufundisha Lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar baada ya Serikali kufikia uamuzi wa kuanzisha somo la Lugha ya Kiswahili katika mitaala ya skuli zote nchini humo.
Alisema, kupitia wadhifa wake wa Ubalozi, atatumia nafasi hiyo kuutangaza uzuri wa Zanzibar nchini humo, ikiwa hatua ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo.
Aidha, alisema Uganda inathamini mchango mkubwa wa wananchi wa Serikali ya Tanzania, hususani katika suala la Ukombozi wa Bara za Afrika pamoja na kuisaidia Uganda katika harakati za kumpindua aliekuwa Rais wa nchi hiyo Dikteta Idd Amin Dada mnamo mwaka 1978.