Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwa namna yoyote kuihusisha Tanzania na Ubaguzi wa aina yoyote au kudai inakiuka msingi ya demokrasia huku ikikandamiza uhuru wa kuabudu ni kituko kipya kuwahi kutokea.
Aidha, CCM imesisitiza kuwa yeyote anayetoa madai hayo, haijui historia ya kweli ya Tanzania mbele ya uso wa dunia.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema wanaodhani watamudu kuipaka matope Tanzania, wajitafakari zaidi.
Mbeto alisema, kama kuna Mataifa Duniani ambayo tokea yapate Uhuru wake yamekuwa yakiongozwa kwa kuheshimu Utawala wa Sheria, Kuenzi Utu, Haki za Binadamu na demokrasia, Tanzania ni miongoni mwa Mataifa hayo.
Alisema, kimsingi na ukweli usiopingika kwamba Tanzania si mshrika wa mapenzi ya jinsia moja, haishabikii ushoga na ubasha, pia haliwezi kuwa Taifa kibaraka lisilo na msimamo imara.
“Tunaelewa kuwa ukitaka mbwa wako afe haraka mpe jina baya. Jaribio lolote la kutaka kuipaka matope Tanzania kwa namna yoyote ya kisingizio cha uvunjaji wa Haki za abinadamu na demokrasia, madai hayo hayana ushahidi wala mashiko,” Mbeto.
Alieleza kuwa, hatua ya chama kimoja cha siasa kususia Uchaguzi Mkuu kwa sababu zao binafsi, kutaka kukinukisha na kukiwasha, hakuhalalishi kuthibitisha madai ya kukosekana utawalabora, demokrasia au kufinya Uhuru wa watu kuabudu.
“Tanzania ni Mwalimu Mkuu wa kufundisha maana ya demokrasia, utawala bora na kuenzi haki za binadamu Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kama wapo wanaopaza sauti zao kwa shinikizo, mihemko na unazi, waache kufanya hivyo,” alieleza.
Pia, Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema, hakuna chama cha Siasa kilichozuiwa kisishiriki Uchaguzi Mkuu au kukamatwa kwa baadhi ya wanasiasa na kuwaweka ndani kimaonevu bila uvunjaji wa sheria za nchi.
“Tanzania si Koloni la Taifa lolote duniani. Limepata uhuru wake baada ya mapambano ya kisiasa yenye hoja na kuanza kujitawala. Tabia ya vitisho, ubabe na mikwala zikome toka sasa,” alifafanua.
Mbeto alisema, iwapo kama kuna baadhi ya Mataifa yalitegemea kuutumia mwanya wa Uchaguzi Mkuu ili Tanzania izame katika ghasia ambazo hatimae zingefanikisha Mapinduzi na kuondoa utawala halali uliowekwa na wananchi, wakajipange upya.
“Hatuwezi kuishi kwa kupimana mbavu kila uchao. Waafrika wameshakataa aina yoyote ya utumwa tokea enzi ya Ukoloni ukiwemo Utumwa wa kudumazwa akili , maarifa na kushindwa kutoa maamuzi,” Mbeto alisema kwa kujiamini.
Kadhalika akitoa mifano hai, Mwenezi huyo alisema Tanzania ndio Taifa pekee duniani lenye raia ambao wanoishi bila kutobaguana kwa rangi,dini na kabila, badala yake watu wake huheshimiana na kuishi kwa upendo.