JUMLA ya taasisi 551 zimeanza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ikiwa ni katika jitihada za kuunga mkono Serikali kupunguza ukataji miti na kulinda afya za wananchi.
Hatua hiyo, ni katika utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za Umma na Binafsi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya mia moja.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis alisema hayo bungeni jijini Dodoma leo Februari 12, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Rungwe Anton Mwantona aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha taasisi zinazohudumia watu wengi zinaweka mifumo ya majiko ya gesi ili kuokoa mazingira.
Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema Serikali tayari imesaini makubaliano ya awali na wawekezaji mbalimbali ikiwemo makampuni ya Oryx, Taifa Gas, Lake Gas na Manji’s gas kuhusu kutoa ruzuku ya Shilingi Bilioni 8.64 kwenye nishati safi ya kupikia.
Khamis alifafanua kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji wa nishati safi ambapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku.
Aidha, alisema Serikali inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa Nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi.