MWENGE wa Uhuru umeingia kwenye Wilaya ya Iramba mkoani Singida kwa ajili ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwa na ujumbe wa kuwasihi wananchi mapambano dhidi ya rushwa, UKIMWI, ulinzi na usalama na utunzaji wa mazingira.
Mwenge huo ulipokewa Julai 24, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda na maelfu ya wananchi na watumishi katika Kijiji cha Ndulungu ukitokea Manispaa ya Singida na kufikia miradi 8 yenye thamani ya Bilioni 12.5.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa daraja la Masagi lililogharimu Milioni 963 likiunganisha Kata ya Mtoa, Mkimbiza Mwenge Kitaifa Wazo Mwang’onda, amesifu utekelezaji wa mradi huo unavyokwenda kufungua fursa za kiuchumi kwa maelfu ya wananchi wa Kata ya Mtoa na Kata jirani katika barabara ya Kibigiri- Masagi hadi Tyeme waliokua wanapata changamoto kwenye eneo hilo.
“Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi huu na kwa kweli tuusifu uongozi wa Wilaya ya Iramba chini ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Mwenda kwa kusimamia mradi huu na miradi mingine ndani ya Wilaya kwa ufanisi mkubwa sana. Nitoe pongezi za dhati kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi na viongozi wa Wilaya na Halmashauri kusimamia kwa ufanisi mkubwa,” alisema.
Mwang’onda baada ya kutembelea daraja na kujiridhisha kisha kuzindua mradi huo.
Aidha, katika Wilaya ya Iramba ambapo Mwenge umekimbizwa takribani KM 174.5 miradi mingine ya kiuchumi, maendeleo na utawala imetembelewa, kukaguliwa ikiwemo ujenzi wa Skimu ya umwagiliaji Masimba katika Kata ya Urughu wa Bilioni 10.49, mradi wa nishati safi ya kupikia wa Milioni 40 na ujenzi wa mabweni mawili, madarasa mawili na matundu 12 Kizaga Sekondari wa Milioni 316.4, ujenzi wa Ofisi ya Kijiji Ndulungu milioni 35 na ujenzi wa zahanati ya Kijiji Ndulungu Kata ya Ndulungu Milioni 225.
Miradi mingine ya maendeleo iliyotembelewa na kukaguliwa ni pamoja na mradi wa vijana wa ujenzi wa kiwanda cha usindikaji wa mafuta ya alizeti cha kikundi cha Ndago Family wa Milioni 28.8 na uwekezaji wa Kitonka Business Centre umegharimu 426.3.