SMZ kushusha bei ya kuunganisha umeme majumbani

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta ya nishati kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa na umeme wa uhakika na wa kuaminika.

Akizungumza leo katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa mfumo wa umeme Zanzibar uliofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Verde, Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Rais Dkt. Mwinyi alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za umeme kwa wananchi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa uzinduzi huo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali katika utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi, sambamba na kuondoa changamoto za kukatika kwa umeme, kupungua kwa kiwango cha umeme katika baadhi ya maeneo na kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kujenga miundombinu mipya ya umeme ikiwemo kuwekeza katika nishati mbadala kupitia jua na upepo, pamoja na kuanzisha mitambo ya usambazaji umeme kwa wananchi. Aliongeza kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo unalenga kuhakikisha takribani wananchi 70,000 wanapatiwa huduma ya umeme.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ipo mbioni kushusha gharama za kuunganisha umeme majumbani kutoka shilingi 200,000 za sasa hadi kufikia shilingi 100,000 pekee.

Vilevile, amefafanua mikakati mingine ikiwemo kuviunganisha visiwa vidogo vya Njau na Kokota na huduma ya umeme, pamoja na kukamilisha mradi mkubwa wa nyaya za umeme wa chini ya bahari (Submarine Power Cable) utakaosambaza nishati kisiwani Pemba.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi kwa Wizara ya Maji, Nishati na Madini pamoja na Kampuni ya NOVASIS International kwa usimamizi bora na ukamilishaji wa mradi huo kwa wakati, huku akiwataka wananchi na wadau kulinda miundombinu hiyo ili ilete manufaa yaliyokusudiwa, sambamba na kuendelea kusimamia miradi mingine ya kimkakati kwa ufanisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here