OWM-TAMISEMI
SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo limeendelea kuimarisha usalama wa wananchi na wafanyabiashara kwa kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kizimamoto Ilala kupata ofisi pamoja na eneo la kuegesha magari kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake katika eneo la Kariakoo.
Hatua hiyo inalenga kuboresha ufanisi wa shughuli za zimamoto na uokoaji, pamoja na kupunguza usumbufu kwa wananchi wakati majanga ya moto yanapotokea katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa kikao kati ya uongozi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kizimamoto Ilala, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA Ashraph Abdulkarim, alisema kuwa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa soko na jamii inayolizunguka.
CPA Abdulkarim aliongeza kuwa ushirikiano huo utawezesha wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kwa amani na utulivu, sambamba na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa bila hofu ya majanga ya moto.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kizimamoto Ilala, SACP Peter Mabusi, amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa kutoa elimu ya kinga dhidi ya moto kwa wafanyabiashara na watumishi wa shirika hilo, pamoja na kufanya ukaguzi wa mifumo ya kuzima moto ili kukabiliana na majanga kwa wakati.
Aidha, Shirika la Masoko ya Kariakoo limekuwa likichangia upatikanaji wa maji kwa ajili ya kudhibiti matukio ya moto kupitia visima vilivyopo ndani ya soko hilo.
Kuanzia mwezi Septemba 2025 hadi sasa, shirika hilo tayari limefanikisha upatikanaji wa zaidi ya lita 134,800 za maji, zilizotumika katika kudhibiti ajali za moto.