Na Albert Kawogo
MKUU wa mkoa wa Geita, Martine Shigela amekemea tabia ya waajiri hususani maofisa utumishi wa ofisi za umma kukwamisha watumishi kubadilisha kada na kupandishwa madaraja.
Shigela ametoa kauli hiyo katika maazimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi, 2026) ambayo kimkoa yalifanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita.
Amesema kazi ya upandishaji madaraja ni endelevu na hivo maofisa utumishi mara kwa mara wanapaswa kupeleka taarifa za watumishi wanaohitaji kupandishwa madaraja kwa hatua zaidi.
“Nielekeze na kumkumbusha RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) jambo hili tuendelee kulifuatilia kwa ukaribu, ili kila mfanyakazi anayestahili kupandishwa daraja aweze kupandishwa”, amesema.
Shigela amesema serikali haitakubali kuona watumishi wa umma waliojiendeleza na wana sifa za kubadili kada ama kupadishwa daraja wanakwamishwa kwa sababu za mtu binafsi.
“Nisisiitize waajiri, tuwape fursa wafanyakazi wetu, wabadilishe kada, kwani inawapa motisha ya kuongeza ari ya kazi na kujituma ili kuongeza juhudi za maendeleo kwenye mkoa wetu.
“Niwasihi na kuwatia moyo watumishi, wanaotamani kubadilisha kada, wajiendeleze kwenye kada ambayo wanataka Kwenda, na kuwasilisha maombi yao kwenye taasisi zinazohusika” amesema.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu imefanikiwa kuwapandisha madaraja watumishi 15,553 tangu ilipoingia madarakani mpaka kufikia Desemba mwaka 2025.
Amesema pia jumla ya wafanyakazi 1,194 wamebadilishiwa kada baada ya kujiendeleza kielimu na wengine kuomba kubadili kada ya utumishi kutokana na kukidhi matakwa ya kitaaluma.