NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Damas Kamani amesema Serikali inasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, jamii na wadau mbalimbali katika kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, ikiwa ni sehemu ya kukuza Uchumi wa Buluu.
Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya miaka 30 ya Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia na Tamasha la Kisiwa cha Mafia 2026 yaliyofanyika katika Fukwe za Bahari eneo la Utende leo Septemba 26, 2026 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani amesema Serikali inawahimiza Wadau wote na jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutumia rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Uhifadhi wa bahari ni msingi mkuu na nguzo isiyoepukika ya maendeleo endelevu ya Uchumi wa Buluu, kwani rasilimali za kwenye maji, yaani bahari, maziwa na mito, haziwezi kuleta tija ya kiuchumi bila kuhifadhiwa ipasavyo,”
Kamani amesema changamoto zikiwemo uvuvi haramu, shughuli zisizofuata taratibu katika maeneo ya hifadhi, mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira, hususan taka za plastiki, zinahitaji ushirikiano wa Serikali, jamii za pwani, wanasayansi, sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo na kuhimiza matumizi ya teknolojia, utafiti na ubunifu katika kuongeza tija kwenye Sekta ya Uvuvi.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo amesema Fursa za bahari zitanufaisha wananchi kwa kufanya uhifadhi wa bahari ambapo wilaya hiyo pia imeshatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na makazi na kueleza kuwa shughuli za utalii wa bahari ambazo ni mazao ya sekta uhufadhi zimechangia Shilingi Bilioni 27 mapato ya halmashauri ya Wiyala hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema asilimia 30 ya mazao ya uvuvi nchini yanachangiwa na bahari ambazo bado ni kidogo ikilinganishwa na malengo yaliyopo, hivyo Serikali itahakikisha inadhibiti uvuvi wa kutumia baruti na uvuvi usiozingatia sheria.