SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kuboresha huduma za mawasiliano katika Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro kupitia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Hayo yameelezwa Juni 3, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama, alipokuwa akijibu swali la Abubakari Asenga Mbunge wa Jimbo la Kilombero kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Dkt. Mkama amesema kuwa kupitia mradi huo, mnara wa mawasiliano ulijengwa katika Kijiji cha Sagamaganga kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.
Aidha, amesema kampuni ya Honora ilijenga mnara wa mawasiliano katika Kijiji cha Mherure ambao mnara huo unahudumia vijiji mbalimbali vinavyozunguka eneo hilo, hatua iliyochangia kuongeza wigo wa huduma za mawasiliano na kuimarisha mawasiliano kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Aprili 8, 2026, UCSAF ilifanya tathmini katika Kijiji cha Mangula B na Kitongoji cha Ikwambi, ambapo ilibainika kuwa Kijiji cha Kanyenja kilijumuishwa katika Mradi wa Mawasiliano Vijijini wa minara 636.
Mnara huo ulijengwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), huku baadhi ya maeneo katika vijiji hivyo yakitarajiwa kujumuishwa katika mipango ya kuimarisha huduma za mawasiliano ili kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma hizo.
Vilevile, Dkt. Mkama amesema Serikali itaendelea kufuatilia ubora wa huduma za mawasiliano katika maeneo husika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na za uhakika.