Serikali yaanza kutoa huduma za wagonjwa wa dharura Nzega Mji

0

Na OR-TAMISEMI

HUDUMA za wagonjwa wa dharura zimeanza kutolewa rasmi katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora baada ya jengo la EMD kukamilika.

Jengo hilo ni miongoni mwa majengo 80 yanayojengwa kwenye Hospitali za Wilaya nchini kote ambapo limekamilika kwa asilimia 98 na kuanza rasmi kutoa huduma.

Akizungumzia ukamilishaji wa jengo hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Dkt. Jabir Juma Msuni alisema Shilingi Milioni 300 zimetumika kukamilisha jengo hilo muhimu ambalo litasaidia kuongeza ubora wa huduma za dharura katika wilaya pia.

“Uwepo wa huduma za dharura utarahisisha utendaji kazi wa watumishi na kuongeza imani kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika hospitali yetu,” alisema Dkt. Jabir na kuongeza kuwa, uwepo wa huduma hizo za dharura zitasaidia kuokoa maisha ya watu kirahisi.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania yamejengwa Majengo ya Huduma za Dharura (EMD) 80 pamoja na Majengo ya Huduma za Wagonjwa Mahututi (ICU) 25 kwenye Halmashauri za kimkakati.

Jumla ya Shilingi Bilioni 203 zimetumika katika ujenzi wa majengo hayo kwenye utoaji wa huduma za afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here