Na WAF, Arusha
NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kusukuma mbele ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Arusha na kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Lengo la kikao ikiwa ni kujadili namna ambavyo Africa CDC itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuunga mkono utekelezaji wa majukumu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Kinara wa Umoja wa Afrika wa masuala ya afya ya mama na mtoto.
Katika kikao hicho, pande zote zimejadili uwezekano wa kuanzishwa kwa sekretarieti maalum itakayoratibu utekelezaji wa ajenda husika.
Sekretarieti hiyo inatarajiwa kufanya kazi kwa ushirikiano kati ya Africa CDC na Serikali ya Tanzania ili kuratibu shughuli zinazohusiana na ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Viongozi hao pia wamejadili maandalizi ya nyaraka na mikakati itakayowezesha kuwasilishwa kwa taarifa za utekelezaji wa ajenda hiyo katika majukwaa ya kimataifa ya afya.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Uteuzi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Kinara wa ajenda hiyo ulipitishwa wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha juhudi za pamoja za Bara la Afrika kwenye kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na huduma za afya ya uzazi barani humo.