Na Rahel Pallangyo
SERIKALI imewataka wachezaji wa timu ya Taifa ya soka ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girl’s kucheza kwa kujituma kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yanayotarajia kuanza kutimua vumbi Oktoba 14 mwaka huu nchini India.
Kauli ya imetolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa katika hafla ya kuwaaga wachezaji wa Serengeti Girl’s wanaokwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kambi katika klabu ya Southampton ya Uingereza kujiandaa na mashindano hayo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mchengerwa alisema wachezaji wanatakiwa kuonesha uzalendo, kujituma, kupambana na kuweka bidii katika michezo hiyo, kwani matarajio makubwa ya Watanzania ni kuona wakifanya vizuri na kufika fainali au nusu fainali na ikishindwa sana ni kucheza robo fainali.
“Mnatakiwa kuweka utaifa mbele na uzalendo na kucheza kwa kujituma kuhakikisha mnafika fainali au nusu fainali ikishindikana basi robo fainali kwani Serikali imeweka mazingira rafiki kwenu,” alisema Mchengerwa.
“Hatuna sababu ya kushindwa, kama wachezaji wakiweka bidii, kuacha uvivu na kujitoka hadi ikiwezekana kuvunjika uwanjani kwa ajili ya kuletea heshima Taifa, Rais wetu Samia Suluhu Hassan na watanzania,” alisema Mchengerwa.
Aliongeza, Serikali imejiridhisha kuwa kambi ya Southampton itakuwa sehemu nzuri kwa timu kupata maandalizi mazuri pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kwenda nchini India katika mashindano hayo.
Upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bima ya Taifa (NIC), Elirehema Doriye licha ya kukabidhi hundi ya Sh milioni 40 na kutangaza bima kwa wachezaji alisema Serengeti Girls wakiingia hatua ya robo fainali watazawadiwa Shilingi Milioni 40, nusu fainali Shilingi Milioni 80 na fainali Shilingi Milioni 100.
Alisema, wachezaji wanapaswa kujituma, kuleta ushindani na kuhakikisha wanashinda katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa sababu hawana cha kuhofia kwa vile wana Bima.
“Jambo la muhimu ni kwenda kupambana sisi kama kampuni ya bima tupo na nyinyi mwanzo mwisho kuhakikisha mnakuwa salama katika suala nzima la bima ya afya,” alisema.
Alisema, jumla ya Dola laki tano na elfu 81 zitatumika katika suala nzima la masuala ua bima kwa wachezaji.
Kocha wa Serengeti Girls, Bakari Shime alisema malengo yao ni kwenda robo fainali katika mashindano ya kombe ya dunia.
“Watanzania wamepania ushindi, kitambaa kizito tuna kazi ngumu ya kuitetea bendera ya Taifa, hii ni mara ya kwanza kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo” alisema Shime.
Alisema, wamejiandaa kwa kadri ya uwezo wao ili kuleta ushindani katika mashindano na watahakikisha wanafikia malengo ikiwemo robo na hata fainali
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB) Felix John ilikabidhi hundi ya Shilingi Milioni 20 na vifaa yaani jezi; truck suit, viatu na soksi zilizoandikwa ‘Visit Tanzania.’