‘Royal Tour’ yaleta Mapinduzi sekta ya Utalii

0
Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA), Richard Rwanyakaato Kiiza.

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Richard Kiiza amesema filamu ya Tanzania The Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii ambapo hadi kufikia nusu mwaka wa fedha wa 2023/2024 mamlaka hiyo imeweza kutembelewa na watalii 534,065.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam Kamishna Kiiza alisema, matarajio ya mamlaka hiyo ni kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024 idadi ya wageni watakaotembelea hifadhi hiyo ifikie milioni moja ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita ambapo wageni kwa mwaka nzima walikuwa 752,232.

Afisa Mawasiliano Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akifafanua baadhi ya mambo katika kikao hicho.

Kamishna Kiiza alisema, ongezeko hilo la wageni linakwenda sambamba na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ambapo mpaka kufikia nusu ya mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya Shilingi Bilioni 123 tayari zimeshakusanywa.

Alisema, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuimarisha usimamizi wa hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ambayo itawawezesha watalii kutembelea maeneo ya utalii bila changamoto.

Kuhusu zoezi la kuhama kutoka ndani ya hifadhi hiyo kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine Kamishna Kiiza alisema, zoezi hilo linaendelea vizuri kutokana na wananchi wengi kuwa na hamasa ya kutaka kuhama hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka imeendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuboresha maisha yao nje ya hifadhi.

Baadhi ya wahariri katika mkutano huo wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia zoezi hilo na kushauri kwamba nguvu kubwa inahitajika kupambana na wale wote wanaotaka kudhoofisha juhudi hizo za serikali zenye lengo la kuimarisha maisha ya wananchi na kulinda hifadhi.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Thobias Makoba ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo hivyo kurahisisha mchakato wa kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Thobias Makoba akizungumza katika kikao kazi hicho.

Makoba alisema, ofisi hiyo imejipanga vizuri katika kuhakikisha kila Mamlaka iliyo chini yake inafanya vikao vya mara kwa matra na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Katika kikao hicho Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitoa taarifa kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusiana na mafanikio ya serikali ya awamu ya sita yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa3 Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Machi, 2021.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here