Na Albert Kawogo
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ikishirikiana na kampuni ya Magazeti ya TSN, itaandaa Jukwaa la Wazi la Ushirikishwaji linalojulikana kama “Fungua Fursa”, litakalofanyika kuanzia Julai 27 hadi 28, 2026, katika mji wa Katoro, mkoani Geita.
Jukwaa hilo linalenga kuwakutanisha wananchi, washirika wa maendeleo, viongozi wa biashara, wawekezaji na viongozi wa serikali ili kujadili na kuonesha fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zinazopatikana katika Mkoa wa Geita.
Akitoa mwaliko kwa wadau kushiriki katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema lengo kuu la jukwaa hilo ni kubaini, kuhamasisha na kutangaza fursa za uwekezaji, biashara na maendeleo zilizopo katika mkoa huo.
Ameongeza kuwa jukwaa hilo pia litatoa nafasi ya kuonesha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Geita, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zilizopo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuchochea maendeleo endelevu ya jamii.
Shighela amesisitiza kuwa Wananchi, wafanyabiashara, wajasiriamali, wawekezaji na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika jukwaa hilo ili kujifunza, kujenga ushirikiano na kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika Mkoa wa Geita.