Na Albert Kawogo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendeleza maridhiano ya kisiasa kuelekea hatua za maboresho ya Katiba kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Julai 30, 2026 alipokutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa nchini, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalihusu maridhiano, mageuzi ya kisiasa, uchumi, huduma za jamii, ajira, uwekezaji na ulinzi wa amani ya nchi.
Akirejea hatua ya mchakato wa maridhiano visiwani Zanzibar, Rais Dkt. Samia aliwaeleza viongozi hao hatua zilizofikiwa za maandalizi ya mchakato wa maridhiano kuelekea hatua zinazofuata za mapitio ya Katiba.
Alisisitiza kuwa, hatua zote za mchakato huo zitafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zilizowekwa, kwa maslahi mapana ya Taifa, na kwamba Serikali itaendelea kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa mazungumzo katika kipindi cha angalau mara tatu kwa kila mwaka.
Mkutano huo, uliowaleta pamoja wenyeviti, makamu wenyeviti, makatibu wakuu na viongozi wa Jumuiya za vyama vya siasa nchini, ni wa pili wa aina hiyo kuitishwa na Rais Dkt. Samia tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mkutano wa awali ulifanyika Machi 31, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wagombea wa nafasi ya Rais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.