Na Mwandishi Wetu, Dar ES Salaam
WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ametembelea mradi wa ujenzi wa matenki maalum ya kuhifadhia mafuta (Oil Terminal) wa TPA unaofanyika katika wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam na kuumwagia sifa utekelezaji wake.
Ujenzi huo unahusisha matenki makubwa 15 yenye uwezo wa kuhifadhi ujazo wa lita 378000 za mafuta pindi yanapoingizwa nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo katika eneo la ujenzi lililopo katika kata ya Tundwi, Prof. Mbarawa alisema ujenzi huo utakaochukua muda wa miaka miwili, utasaidia katika kuboresha ufanisi wa bandari na kupunguza foleni ya meli za kupakua mafuta, ambapo meli moja hutozwa wastani wa faini ya Shilingi Milioni 50 kwa siku moja wakati ikiwa katika foleni ya kupakua mafuta hayo.
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa, ufinyu wa matenki ya kuhifadhia mafuta ulisababisha wasafirishaji kutozwa kiasi kikubwa cha pesa na mwisho wa siku gharama hizo pia ziliwagusa wananchi.
“Wakati mwingine meli hulazimika kusubiri kupakua mafuta hata zaidi ya wiki moja, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani wasafirishaji wa mafuta wanaumia na faini hii,” alisema Prof. Mbarawa.
Alisema, ili kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa moja ya bandari zenye ushindani duniani, Serikali imeamua kufanya ujenzi huo wa matenki 15 ambao sasa meli hizo zitatumia masaa machache kupakua nishati hiyo na kuondoka.
Pia, ujenzi huu utafanya kazi ya usambazaji wa mafuta hayo kwenda kwa wateja ( makampuni ya kuuza mafuta) kwa urahisi sana na kukabiliana na uhaba wa mafuta unaoweza kutokea.
Alisema, ujenzi wa matenki hayo utaifanya Serikali kuwa na hifadhi ya kutosha ya nishati hiyo kwa ajili ya usalama wa nchi. “Nikiwa kama Waziri wa Uchukuzi, nimefurahi sana kuona mradi huu hatimaye unatekelezwa na naupongeza sana uongozi wa TPA kwa hatua hii,”
“Tulijaribu mara kadhaa huko nyuma lakini tulishindwa, ila mipango thabiti ya bodi na uongozi wa TPA umepelekea kutekelezwa kwa mradi huu,” alisema Prof. Mbarawa.
Meneja wa mradi huo Injinia Hamis Hassan Mbutu alisema, unatarajiwa kumalizika kwa wakati na kuwa na tija kwa bandari hiyo na Serikali kwa ujumla katika kukusanya ushuru.
Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Prof. Mbarawa, Mkurugenzi Msaidizi wa TPA Juma Kijavara alisema, mkataba wa ujenzi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 678.6 ulisainiwa rasmi Februari 26, 2024, ambapo tayari Mkandarasi China Railway Major Bridge Engineering Group ameshalipwa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.9 kuanza ujenzi huo.
Akimuelezea Profe. Mbarawa hatua za utekelezaji wa mradi huo, Injinia Wen Hongyuan kutoka China Railway alisema, kwa sasa upo katika asilimia 5 ya utekelezaji, ambapo tayari kazi ya kusafisha eneo la ujenzi na ofisi za wajenzi zimekamilika.
Kuhusu mgawanyo wa matenki hayo, Injinia Wen Hongyuan alisema ujenzi huo utahusisha matenki 6 kwa ajili kuhifadhia mafuta aina ya Diesel, matenki 5 ya kuhifadhia Petroli na matenki matatu kwa ajili ya kuhifadhia mafuta ya kuendeshea ndege.