Pinda aingia mtaani kutatua migogoro ya ardhi

0

Na Munir Shemweta, WANMM

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda ameingia kutatua na kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake ya migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma.

Pinda katika ziara yake hiyo Januari 11, 2024 aliambatana na watendaji wa sekta ya ardhi Makao Makuu ya Wizara, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma na wale wa Jiji la Dodoma ambapo alitembelea eneo la Chang’ombe.

Naibu Waziri wa Ardhi alianza ziara yake kwa kutembelea eneo la Chang’ombe Mbwanga ambapo Bi. Dorothy alibomolewa kimakosa ukuta wa nyumba yake na halmashauri ya jiji la Dodoma, ambapo Pinda alielekeza mwananchi huyo kujengewa ukuta huo.

“Ninyi mnaoishi hapa sura ya ujirani lazima itengenezwe kwa kuepuka migogoro ya ardhi katika maeneo yenu, mnataka mpaka Waziri aje ndiyo atengeneze ujirani” alisema Pinda.

Aidha, alitembelea eneo la Chang’ombe Extension, ambapo mwananchi mmoja Ramadhani Kisiju anadai kumiliki kiwanja alichokuwa akilima kwa muda mrefu.

Katika kutafuta suluhu ya eneo hilo, Pinda aliagiza mmiliki wa eneo analodai Kisiju kumiliki afike ofisini kwake na nyaraka zote za umiliki kwa lengo la kupata muafaka wa mgogoro huo.

“Kitu kimoja ninachotaka kukusaidia mzee wangu, ngoja tukaangalie hiki kiwanja uhalali wake halafu baadaye tutakupa majibu,” alisema Naibu Waziri wa Ardhi.

Uamuzi wa Pinda kutembelea na kukagua maeneo ya mgogoro uwandani unafuatia kuwasilishwa kwa malalamiko ya migogoro ya ardhi kwake huku baadhi ya malalamiko yakihusisha watendaji wa sekta ya ardhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here