Ni lazima Uturuki iendelee kuwa mwanachama wa NATO?

0

Na Prof. Dkt. Kudret BULBUL

KATIKA siku za hivi karibuni, upinzani unaoongezeka siku hadi siku ambao Uturuki inauonyesha kuhusiana na mfumo wa ulinzi wa anga S-400, pamoja na kupinga Marekani na Syria kushirikiana na vikundi vya kigaidi, kumesababisha yazuke maswali juu ya ushiriki wa Uturuki katika Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi (NATO).

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence aliwahi kusema, Uturuki inabidi ichague iendelee kubaki kama mshirika muhimu wa jeshi la kujihami la NATO au inataka kuvuruga ushirikiano kwa kufanya maamuzi yasiyokuwa ya busara yatakayouweka hatarini ushirikiano baina yao.

Hayo yalijibiwa na Makamu wa Rais wa Uturuki, Fuat Oktay ambaye alisema Marekani inabidi ifanye maamuzi kama inataka kuendeleza urafiki na Uturuki au iwasaidie magaidi na kudhoofisha ulinzi wa mshirika wake wa NATO na hivyo kuweka rehani urafiki baina ya Mataifa hayo.

Kwanza kabisa, tuweke wazi kwamba ni Marekani pekee ndiyo inayohoji uanachama wa Uturuki katika jeshi la NATO na sio uongozi wa umoja huo wala wanachama wengine. Nchi za Kifashisti za Ulaya zilipoteza vita ya pili ya dunia, nchi za kidemokrasia zilishinda vita hivyo.

Baada ya vita hivyo, michakato ya kidemokrasia ilianza kuenea dunia nzima. NATO ambayo ilianzishwa baada ya vita ilianzishwa na nchi za kidemokrasia. Kutokana na vitisho na mahitajio ya wazi iliyoonyesha Urusi dhidi ya eneo la Bosphoros la Uturuki, mwaka 1945, Uturuki ikataka kuwa sehemu ya umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi, NATO.

Mchakato uliokuwapo baada ya vita ya pili ya dunia na pengine tunachoweza kusema ni mchango muhimu wa NATO kwa Uturuki, ni nafasi ya umoja huo katika kufanikisha Uturuki kuingia katika demokrasia. Kwa miaka hiyo kama yasingekuwapo masharti kutoka nje, basi kuna uwezekano demokrasia ingechelewa kuanza kutumika nchini Uturuki.

Kipindi cha vita baridi, NATO iliihakikishia usalama Uturuki dhidi ya vitisho vya Urusi. Pamoja na michango chanya muhimu kabisa iliyotajwa hapo juu NATO imeigharimu Uturuki kwa kiasi kikubwa. Kwa utawala wa kiuangalizi ulioundwa mwaka 1960 baada ya mapinduzi, NATO na haswa haswa Marekani ilipata nafasi ya kuitawala Uturuki.

Makundi kama ‘Gladio’ lililopo Italia yanayohusishwa na NATO, inasemekana yapo pia katika nchi nyingine wanachama wa NATO. Katika mapinduzi ya Uturuki ya mwaka 1980, itakumbukwa aliyekuwa Rais wa Marekani kipindi hicho alinukuliwa akisema “vijana wetu wameshinda”. Mwisho mapinduzi ya FETO ya Julai 15, watu wengi wanayahusisha na Marekani.

MCHANGO WA UTURUKI KWA NATO

Tukianza na tangu ulipoasisiwa umoja wa NATO, katika vita nyingi au misheni ambazo umoja huo umekuwa ukishiriki askari jeshi wa Uturuki wamekuwa pia wakitumika. Moja ya vita ambazo Uturuki ilipoteza askari wengi ni vita ya Korea, ambayo inaweza kuwa mfano mzuri wa ushiriki wa askari wa Uturuki katika vita vya NATO.

Mume wa shangazi yangu ambaye pia ni mjomba wangu, ni katika waliopata kilema katika vita vya Korea. Wakati wa vita vya Afghanistan mwaka 2012 chini ya Uturuki ilishiriki chini ya mwamvuli wa NATO (ISAF), kutokana na helikopta kuanguka rafiki yangu wa karibu Meja Sukur Bagdatlh alipoteza maisha. Nichukue nafasi hii kuwaombea rehma wote wawili.

Lakini, mchango halisi wa Uturuki kwa NATO ni haswa katika kuleta uhalali wa umoja huo kufanya oparesheni katika Mataifa ya Kiislamu. Mara zote NATO imekuwa ikipingwa kwa minajili kwamba, uwepo wake katika Mataifa ya Kiislamu ni sawa na kuweka utawala mwingine wa kimabavu au kuanzisha vita nyingine. Sasa NATO bila Uturuki itakumbana na aina hii ya upinzani.

Ukiangalia katika karne ya 20 Mataifa yaliyokuwa yakiongoza kwa ustawi utaona ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Marekani, Urusi na Dola la Othomani. Katika karne ya 21 siasa ya dunia inaongozwa na Mataifa hayo hayo. Katika Mataifa hayo sehemu ya dola la Othomani unaweza kuziongeza Uchina na Uturuki.

Kihistoria Uturuki ni moja katika Mataifa viongozi yanayoanzisha mchezo. Uturuki ni Taifa pekee katika Umoja wa NATO ambalo watu wake ni waislamu. Uturuki iliialika Uhispania ili kwa pamoja nchi hizo mbili ziongoze shirikisho la tamaduni na matokeo yake ndio tamaduni zilizopo hivi sasa.

Ni kwa sababu hiyo Uturuki haichukuliwi wala haionekani kama Mataifa mengine ya Magharibi, bali wanachama wa kawaida wa NATO. Ushirikiano na mchango ilioutoa Uturuki kwa NATO, hauwezi kulinganishwa na mchango wa Mataifa kama Ugiriki, Italia na mengineyo.

Iwapo Uturuki itachukuliwa kawaida kama Mataifa mengine ya Magharibi, basi NATO pia haitaweza kuchangia vya kutosha katika amani ya ulimwengu. Kutokana na kina chake cha kihistoria, uwezo na mchango wake katika kuchangia amani ya kiulimwengu Uturuki kama vile ilivyo kwa NATO, ni lazima idumishe mahusiano madhubuti na Urusi, Magharibi, Mashariki, Kaskazini, Kusini na katika kila pembe. Kwa Uturuki mahusiano hayo sio masuala ya kuchagua.

Kwa wanaotetea kwamba NATO ni kitu cha lazima kwa Uturuki wanaweka msisitizo kwamba, ni NATO ndiyo inaweza kuleta msawazo baina ya Kanda na Urusi. Wanalazimisha kwamba Uturuki bila NATO itakuwa katika tishio lililokuwapo hapo mwanzo dhidi ya Urusi.

Bila shaka msisitizo huu ni sawa. Pamoja na hilo, tishio la huko nyuma la Urusi na msaada wa NATO kwa Uturuki haviwezi kusemwa kwamba vilikuwa ni hitajio la Uturuki pekee. NATO haikuisaidia Uturuki kwa vile Uturuki ilikuwa ikihitaji msaada, bali iliisaidia ili kuweza kupunguza shughuli za Urusi ambazo zilikuwa zikitishia maslahi yake.

Yaani, hata kama Uturuki isingekuwa mwanachama wa NATO, bado NATO ingelazimika kwa namna moja au nyingine kuisaidia Uturuki. Mfano, leo hii India sio mwanachama wa NATO, lakini tunaona Marekani ikilisaidia Taifa hili kuliko Taifa jingine lolote mwanachama wa NATO, kwa kuwa lengo ni kuzuia kuenea shughuli za China.

Kwa kifupi NATO ambayo inataka idiolojia zake zienee na zidumu katika ngazi ya ulimwengu pamoja na kuizunguka China na Urusi na Mataifa mengine, haina budi kusaidia Mataifa mengine yawe au yasiwe mwanachama wa NATO. Uwepo wa Uturuki ndani ya NATO ni suala ambalo lazima liendelezwe.

Marekani na NATO wanapojaribu kuweka mipaka mipya Mashariki ya Kati, au wanapojaribu kuwaimarisha magaidi waliopo karibu na mipaka ya Uturuki, wasitegee kwamba Uturuki itakaa kimya. Wasiiotee ndoto, Uturuki ya aina hiyo. Mataifa kama India, Indonesia, Brazil, Malesia, Pakistani, China na mengine kama hayo sio wanachama wa NATO lakini, ni Mataifa ambayo siku hadi siku yanajipanua kisiasa.

Uturuki ni katika Mataifa ambayo yanaweza kupanga mustakabali wake. Tumalizie na maneno ya kihistoria ya Ismet Ininu, ni maneno ambayo mwaka 1964 aliyaongea kutokana barua ya Johnson: “Dunia mpya inaanzishwa upya na Uturuki itachukua nafasi yake katika dunia hiyo. Hata kama bila NATO Uturuki itapoteza baadhi ya vitu, lakini inaweza kuendelea na safari yake. Pamoja na hayo NATO bila Uturuki haitakuwa imepoteza kitu kidogo.”

*Mwandishi wa Makala hii ni Mkuu wa kitivo cha siasa Chuo Kikuu cha Ankara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here