Mshomba: Tamasha la Kizimkazi ni fursa kwa NSSF

0

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba amesema, Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2024 kwa upande wa NSSF ni fursa kwa sababu yanakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema, Mfuko unapata fursa ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi pamoja na kuangalia fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwekezaji

Mshomba alisema hayo, mara baada ya kufungwa kwa mafunzo ya Tamasha la Kizimkazi 2024, yaliyofanyika katika Uwanja wa Mwehe, Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, 20 Agosti, 2024.

Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, ambapo Mfuko ulitoa hundi ya Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za kilimo biashara.

Alisema, NSSF inatumia fursa ya uwepo wa matamasha kama la Kizimkazi kwa sababu ina jukumu la kuifikia sekta rasmi na sekta isiyo rasmi ambayo imebeba kundi kubwa likiwemo la wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiriamali wengine.

Mshomba amewahakikishia Watanzania kuwa, NSSF imedhamira kuwafikia wajasiriamali waliopo maeneo mbalimbali nchini, ili kuwapatia elimu ya hifadhi ya jamii na kujiunga na Mfuko.

“Nazidi kuwahakikishia Watanzania kuwa NSSF tuna dhamira ya dhati ya kuwafikia vijana hususan wajasiriamali nchini nzima na kuwapa elimu ya hifadhi ya jamii, kuwaandikisha ili waweze kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye,” alisema Mshomba.

Alisema, NSSF itaendelea kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali yaliyopo katika sekta binafsi na sekta isiyo kwani hiyo ndio azma ya msingi ya kuandikisha Watanzania wengi ili wanufaike na sekta ya hifadhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here