Na Iddy Mkwama
KWA miaka mingi, Serikali ya Tanzania na Ujerumani zimekuwa na ushirikiano wa moja kwa moja kwenye masuala mbalimbali; hiyo ni mbali na manufaa mengine ambayo nchi inanufaika kupitia program za Kimataifa ambazo nchi hiyo inachangia.
Ni program zinazosimamiwa na Mashirika kama Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kusimamia fedha zinazotolewa kusaidia shughuli za maendeleo kwenye nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Ushirikiano huu una historia ya muda mrefu na mizizi ilijengwa katika msingi wa urafiki kati ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Prof. Bernhard Grizmek, aliyekua Rais wa Shirika la Kiserikali la Uhifadhi wa Wanyamapori (Frankfurt Zoological Society) lenye Makao yake Makuu nchini Ujerumani.
“Napenda kushukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huu na kwa mchango wao mkubwa kwenye sekta ya uhifadhi nchini,” anasema Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Hazara Chana.
Dkt. Chana alitoa kauli hiyo Disemba 2, 2024 wakati wa hotuba yake kwenye hafla ya kupokea magari na mitambo ambayo imetolewa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kupitia Mradi wa kupunguza athari za UVIKO 19 “Emergency and Recovery Support for Biodiversity Tanzania (ERB)” ambao upo chini ya Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).
Katika hafla hiyo ambayo mbali na kuhudhuriwa na maafisa mbalimbali wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, George Waitara, mwakilishi wa Balozi wa Ujerumani nchini Julia Kroberg, mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) Jennifer Woelf na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).
Waziri Dkt. Pindi Chana anasema, gari na mitambo hiyo ina thamani takribani Shilingi Bilioni 6.4 za Kitanzania, ambapo ni maroli nane na mitambo mitano ambayo imetolewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi, utalii na kijamii na vifaa hivyo vitatumika kwenye hifadhi ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la akiba la Selou.
“Tumepokea, tumepewa dhamana kwa niaba ya watanzania Milioni 62, nawahakikishia vifaa hivi na miradi mingine itasimamiwa kwa umakini,” anasema Waziri Chana na kuongeza kuwa, mbali na kupokea maroli hayo na mitambo, kwa kupitia mradi huo, yatanunuliwa matrekta, kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya barabara, gari (basi) litakalotumika kutekeleza shughuli za ujirani mwema, kununua ndege, boti za doria na miundombinu ya mawasiliano na nishati.
Anasema, Ujerumani inashirikiana na Tanzania kupitia usaidizi unaotolewa kwa Mashirika ya Kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika. Aidha, Serikali ya Ujerumani imekuwa mojawapo ya washirika wakuu wa Tanzania katika uhifadhi wa bioanuwai katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba.
“Napenda kuwahakikishia kuwa, vifaa na fedha za mradi huu na miradi mingine ya wafadhili zitaendelea kusimamiwa kikamilifu na kutumika kwa shughuli zilizokusudiwa ili kuboresha na kuimarisha juhudi za uhifadhi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema Waziri huyo wa Maliasili na Utalii huku akipongeza hatua ya mashirika ya ndege kutoka Ujerumani ambayo yanafanya safari zake nchini na kuleta watalii na wafanyabiashara.
Aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania inathamini uungwaji mkono wa Serikali ya Ujerumani kupitia mradi huo wa ‘Emergency and Recovery Support for Bioviversty in Tanzania’ wenye thamani ya Euro Milioni 20 na nyongeza kiasi cha Euro Milioni 15 ili kukabiliana na athari za UVIKO – 19, ambapo mikataba ya utekelezaji wake ilisainiwa Oktoba 2021 na Machi 2024.
Aidha, taarifa zaidi zinaonyesha kuwa, Serikali ya Ujerumani inatekeleza mradi huo ikiwa ni ahadi ya Kansela wa zamani Angela Markel, aliyoitoa katika mkutano wa Tisa wa nchi wanachama (conference of Parties – CoP) wa mkataba wa uhifadhi wa bioanuwai uliofanyika mjini Bonn, mwaka 2008.
Kupitia ahadi hiyo, kuanzia mwaka 2013, kiasi cha Euro 500 kimekuwa kikitolewa kila mwaka kwa ajili ya uhifadhi wa misitu na mazingira mengine duniani kote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA George Waitara anasema, wao wana miradi minne ambayo inatekelezwa katika hatua mbalimbali ukiwemo wa kupunguza athari za UVIKO – 19.
“TANAPA kama ilivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaiona na kuitambua Ujerumani kama mshirika muhimu na ilifanya maamuzi sahihi kwa kupitia msaada huu wa dharura ambao ulikuja wakati mgumu wa mlipuko wa UVIKO – 19, ambapo maeneo ya uhifadhi yalipoteza mkondo wa mapato ambao kwa kawaida uliyatumia kujiendesha,” anasema Waitara.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Ujerumani kukabidhi magari kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia sekta ya Utalii, Novemba 14, 2024, KfW walikabidhi msaada wa magari mawili (2) aina ya ISUZU FVZ yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 600 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Selous.
Mbali na msaada huo, Disemba 20, 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokea magari 51 na kuweka wazi kwamba, ufadhili huo utasaidia kuongeza wigo wa utekelezaji wa shughuli muhimu za uhifadhi na utalii zinazoendelea katika maeneo mengine yaliyohifadhiwa na kuchangia lengo la kuhifadhi mifumo muhimu ya ikolojia kwa manufaa ya wanadamu.
“Miradi hii siyo tu inaimarisha uhusiano uliopo kati ya Serikali hizo mbili katika kusaidia sekta mbalimbali, bali pia ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa siku zijazo kati ya Tanzania na Ujerumani kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa bioanuwai kwenye mifumo ikolojia ya maeneo ya hifadhi za Taifa,” anasema.
“Nachukua fursa hii kutoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi na Wakuu wa Mashirika ya TANAPA na TAWA kuhakikisha msaada huu wa vitendea kazi unaenda kufanya kazi zilizokusudiwa za uhifadhi wa maliasili na utalii na kwamba vitendea kazi hivi vitumike na kutunzwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya matumizi ya mali za Serikali.” anasema Waziri Mkuu, agizo ambalo lilirudiwa na Dkt. Pindi Chana hivi karibuni.
Hakika, kama anavyosema Mwenyekiti wa bodi kwamba, Ujerumani ni mshirika muhimu katika kusaidia sekta ya utalii nchini, bado naamini kwamba mbali na misaada hiyo ambayo inaendelea kutolewa kupitia mradi wa ERB, bado kuna fursa nyingine zaidi zinazopatikana kwenye nchi hiyo na nchi inaweza kuzitumia.
Miongoni mwa fursa hizo ni suala la utalii wa matibabu, ambalo ni eneo jipya lililoanza kutekelezwa nchini, lakini wao wamefika mbali na wananufaika na utalii huo kutokana na mfumo wao wa huduma za afya
Taarifa zinaonyesha kuwa, kwa mwaka Ujerumani wanaingiza Euro Bilioni 1.2 kutokana na utalii wa matibabu na nchi ambazo zinaongoza kwenda nchini humo kwa ajili ya utalii wa matibabu ni Urusi, Romania, Ufaransa, Bulgaria, UAE, Saudi Arabia na Kuwait.
Huduma ya afya ya Ujerumani inatajwa kuwa bora zaidi katika Ulaya na duniani kote na ndiyo sababu nchi hiyo inapokea idadi kubwa ya wageni kila mwaka na inajulikana kama ‘Hospitali ya Ulaya.’
Kwa maana hiyo, kwa kutumia ushirikiano wa kihistoria tulionao, tunaweza kunufaika kwa kupata uzoefu zaidi kwenye eneo hilo la utalii na inaweza pia kusaidia kuboresha huduma za afya nchini.